Mshambuliaji mweledi wa timu ya taifa ya Togo, Kossi Kuodagba aaga dunia

Mshambuliaji wa Togo, Kossi Kuodagba ambaye alirejea nyumbani kwa mintarafu ya marufuku ya kutoka nje anaripotiwa kuaga dunia nyumbani kwake baada ya kuugua malaria.

Mchezaji huyo wa ASC Kara, alimaliza msimu wa ligi ya Togo kama mtungaji bora wa mabao kwa miaka miwili mfululizo na kusaidia klabu yake kushinda taji la ligi mwaka 2019.

Kulingana na nduru za habari Kossi aliondoka Kara huku msimu huu ukisimamishwa kwa muda kwa sababu ya janga la virusi vya corona ili kuishi na jamaa zake eneo la Devie.

Inaripotiwa kuwa nguli huyo wa miaka 25 aliugua malaria akiwa jijini Lome na kisha kuaga dunia.

Togo FA ilitoa taafira kuthibitisha kifo cha Koudagba na kumuomboleza kama mchezaji bora uwanjani na pia nje.

"Katika hali hii ya uchungu, Kamati Kuu ya FTF ingependa kutambua kumbukizi za mchezaji huyo,ambaye umahiri wake nje na ndani ya uwanja inatambulika kote."

Pia walituma risala za rambirambi na kusema wamempoteza gwiji na mchezaji bora,

"Kamati Kuu ya FTF kwa niaba ya shirikisho la soka la Togo, ingependa kutuma rambi rambi kwa familia ya mwendazake, wapendwa,klabu ya ASCK pamoja na wachezaji wa timu ya taifa ya Togo."

Kossi alikuwa anatazamiwa kujiunga na klabu ya Tunisia, US Tataouine mwaka jana lakini alishindwa kwa sababu ya matatizo yake ya moyo.

Alishiriki mechi tatu za timu ya taifa na alihusishwa katika kikosi cha mchuano wa Kombel la Mataifa ya Afrika 2019.