Manchester United kushikilia nafasi ya tano baada ya mchuano wao na Southampton

Mechi kati ya Manchester United na Southampton ilivunja matumaini ya mashetani wekendu kuwa katika nafasi ya tatu katika jedwali huku wakitoka droo ya 2 kwa 2 baada ya mechi kukamilika.

Mabao mawili ya mapema kutoka kwa Marcus Rashford na Anthony Martial hayakutosha United kuzoa alama zote tatu huku Obafemi akifunga bao dakika za mwisho na kuhakikisha kuwa mechi hiyo inakamilika sare.

United walilazimika kutafuta bao katika mechi hiyo ya Jumatatu, Julai 13 usiku, ili kuwa kifua mbele baada ya Stuart Armstrong kufungua ukurasa wa bao katika dakika ya 12.

Juhudi za Marcus Rashford za kuwafungia United bao dakika 16, zilikataliwa huku akidhani amefunga bao lake.

Huku akipiga moyo konde, Muingereza huyo alitingisha wavu na kupata bao la kusawazisha dakika ya 20, kwa kupiga mkwaju kupitia mguu wake wa kushoto akiwa mbali na kona.

Martial aliwaongezea wenyeji bao lingine dakika tatu baadaye huku akiweka kimyani kombora lililompita McCarthy na kumalizia vyema pasi ya BrunoFernandes.

Awamu ya pili iliwashuhudia Saints wakitumia vizuri nafasi ya United kulaza damu na kuadhibu vijana wa Ole Gunnar Solskjaer huku Obafemi akifunga bao la kusawazisha dakika za mwisho.

Matokeo hayo yana maana kuwa klabu ya Manchester kwa sasa imeshiriki mechi 18 bila kushindwa lakini walipoteza nafasi murwa ya kumaliza miongoni mwa timu nne bora.