Arsenal yainyuka Chelsea na kuweka rekodi ya mataji 14 ya kombe la FA

aubameyangl
aubameyangl
Arsenali ilitoka nyuma na kuilaza Chelsea mabao mawili 2-1 katika fainali ya kombe la FA, na kuweka rekodi mpya ya kunyakua taji la 14. Nahodha wa Arsenali  Pierre Emerick Aubameyang alisawazisha katika kipindi cha kwanza kabla ya kufunga goli la ushindi kunako kipindi cha pili.

Christian Pulisic alikua ameiweka Chelsea mbele katika dakika la tano. The gunners sasa wamefuzu kwa kombe la ligi la Uropa, katika msimu wa kwanza wa kocha mkuu Mikel Arteta.

Kocha wa Arsenali Mikel Arteta anadai watafanya mazungumzo na nahodha Pierre Emerick Aubameyang kuandikisha mkataba mpya ugani Emirates, ili kuendeleza kazi yake nzuri. Mzaliwa huyo wa Gabon amesalia na mwaka mmoja katika kandarasi yake na anamezewa mate na miamba wa Uhispania,  Barcelona. Aubameyang amefunga jumla ya magoli 29 msimu huu na kuwasaidia kushinda taji la FA.

Kocha wa Chelsea Frank Lampard anadai hakufurahishwa na refa kumpa kiungo Matteo Kovacic kadi nyekundu katika fainali ya FA dhidi ya Arsenali jana. Lampard anaamini Kovacic hakucheza visivyo na ange faa angalau kadi manjano, kwani kutoka kwake katika mechi kulihujumu mipango yao. The blues walipoteza 2-1 na sasa watajiandaa kwa mechi ya mkondo wa pili wa klabu bingwa bara Ulaya dhidi ya Bayern Munich baada ya kupoteza 3-0 katika awamu ya kwanza.

Mabingwa wa Italia Juventus walinyukwa 3-1 dhidi ya Roma mjini Turin na kupoteza rekodi ya kutofungwa nyumbani katika mechi 39. Juve ambao tayari walikua wamenyakua taji la serie A walipumzisha wachezaji kadha akiwemo mfungaji bora Cristiano Ronaldo. Katika mechi nyingine za Italia, Inter Milan ililaza Atalanta 2-0, Napoli ilibwaga Lazio 3-1 huku AC Milan ikicharaza Cagliari 3-0.

Kwingineko,  Eddie Howe amejiuzulu kama kocha mkuu wa klabu ya Bournemouth baada ya kuhudumu kwa miaka 12. Mzaliwa huyo wa Uingereza mwenge umri wa miaka 42 anadai atapumzika kwa muda kabla ya kurejea katika ukufunzi.

Huku nyumbani, afisa mkuu mtendaji wa FKF Barry Otieno amekiri mahakama ya leba ya  imefunga akaunti za shirikisho hilo. Haya yanajiri baada yao kukosa kumlipa kocha wa Harambee stars wa zamani Bobby Williamson zaidi ya shilingi milioni 50 kama fidia ya kumchuja kazi kabla ya kandarasi yake kukamilika mwaka  2015. Muingereza huyo alilishtaki shirikisho hilo  namahakama iliagiza alipwe hela zake . Barry hata hivo anaamini watafikiana makubaliano na mawakili wake Williamson ili waweze kutatua  suala hilo nje mahakama.