Arsenal yalaza Liverpool na kutwaa ubingwa wa taji la Community Shield

arsenal
arsenal
Arsenal iliwafunga mabingwa wa ligi ya Uingereza Liverpool 5-4 kupitia mikwaju ya penalty, na kunyakua kombe la Shield, baada ya kutoka sare ya 1-1 ugani Wembley.

Nahodha Pierre-Emerick Aubameyang aliweka mabingwa hao wa kombe la  FA kifua mbele kunako dakika ya 12, kabla ya Takumi Minamino kusawazishia the reds katika dakika ya 73. Nguvu mpya Rhian Brewster wa reds alipoteza nafasi yake kabla ya Aubamayang kufunga penalty ya ushindi.

Hayo yakijiri, mlinzi wa Arsenal Maitland-Niles na Conor Coady wa Wolves wameitwa katika kikosi cha Uingereza kitakachopambana na Denmark na Iceland katika mechi za Nations League mwezi ujao. Wawili hao ambao wameitwa kwa mara ya kwanza katika kikosi cha Gareth Southgate wamefanya idadi ya wachezaji kuwa 25 huku wawili wakitarajiwa kuchujwa licha ya hofu ya kuwa wachezaji kadha wamewekwa katika karantini kutokana na janga la corona.

Katika mchezo wa tenisi, Naomi Osaka alijiondoa kutoka kwa fainali ya michuano ya tenisi ya Western and Southern Open baada ya kupata jeraha la msuli, siku mbili kabla ya mechi za US Open kuanza. Mzaliwa huyo wa Japan alifaa kucheza dhidi ya Victoria Azarenka wa Belarus jijini New York kabla ya kujiondoa na kupelekea Azeraka kupewa taji hilo. Osaka amepangiwa kucheza na  Misaki Doi katika awamu ya kwanza ya US Open kesho.

Kwingineko, bingwa wa dunia Lewis Hamilton alishinda majaribio ya mwisho ya mbio za langa langa za Ubegiji huku mwenzake wa Mercedes Valtteri Bottas akimaliza wa pili na Max Verstappen wa Red Bull akimaliza wa tatu.  Muingereza huyo atakua anawania kushinda taji la tatu mfululizo msimu humu katika fainali ya mbio hizo leo.