Kapu la soka: Man City wawania kusalia kileleni, Harambee Starlets wachanjwa

harambee starlets wachanjwa
harambee starlets wachanjwa

Manchester City watakua wanawania ushindi ili kusalia alama14 kileleni mwa ligi ya EPL kwa ushindi dhidi ya Leeds United huku ligi ikiingia mechi ya 31 leo.  

Mabingwa watetezi Liverpool nao watakabana koo na  Aston Villa huku Chelsea wakizaragazana na Crystal Palace.

Hapo kesho mechi ya kukata na shoka kati ya Manchester United na Tottenham itachezwa London huku kocha wa United  Ole Gunnar Solskjaer akiwania kulipiza kisasi baada ya kulazwa 6-1 katika mkondo wa kwanza.

Arsenal nao watachuana na Sheffield huku Leicester ikicheza na Westham.

Mlinzi wa zamani wa Manchester United Gary Neville anadai klabu hio inafaa kumsajili mlinzi wa Real Madrid Raphael Varane mwishoni mwa msimu ili kuongeza matumaini yao ya kushinda mataji.

Mfaransa huyo ana uzoefu mkubwa kwani ameshinda kombe la dunia, mataji manne ya ligi ya Uhispania  na manne ya igi ya mabingwa.  

Neville anaamini uzoefu wa Varabe utawapa United fursa dhabiti zaidi katika  kitengo cha ulinzi ambacho kimekua kikisuasua. Varane amesalia na miezi 18 pekee katika kandarasi yake na huenda Madrid wakaamuuza ili kupata senti za kusajili mshambulizi.

Kocha wa zamani wa  Harambee Stars Rishadi Shedu anaendelea kupata nafuu akiwa katika hospitali moja mtaani Eastleigh, jijini Nairobi baada ya kupatikana na virusi vya corona. Madaktari wanasema Shedu ambaye pia anaugua asthma anaendelea vyema na huenda akaondoka baada ya siku kumi au zaidi.

Kocha huyo mkongwe hapo awali aliongoza Bandari, na KCB na alikuwa kwenye kitengo cha ukufunzi cha Stars kutoka mwaka 1994 hadi 2010 na pia kuwafunza kinda wasiozidi umri wa miaka 17-23.

Wachezaji wa Harambee Starlets pamoja na maafisa wa kitengo cha ufundi walipata chanjo ya Covid-19 jana huku shirikisho la soka nchini  FKF na wizara ya michezo wakifanya harakati ili ligi kuu nchini iweze kurejea.

Timu za ligi ya FKF za jijini Nairobi zitapata chanjo leo zikifuatwa na timu za kaunti tofauti nchini. Haya yanajiri siku mbili baada ya FKF kuomba serikali kupitia wizara ya michezo kuwapa fursa ya kurejea viwanjani kwani wana uwezo wa kufuata kanuni za covid-19 na kuzuia maambukizi zaidi.