Mashindano ya kuwania kombe la ligi ya mabingwa (Champions League) yaliingia katika raundi ya tatu kwenye hatua ya makundi siku ya Jumanne.
Timu zilizo kwenye kundi A, B, C na D zilicheza mechi zao siku ya Jumanne ilhali timu zilizo kwenye kundi E, F, G na H zillicheza usiku wa Jumatano.
Mechi mbili za ufunguzi usiku wa Jumatano zilikuwa kati ya miamba wa soka nchini Uhispania Barcelona na Dynamo Kyiv ya Ukraine na nyingine kati ya Salzburg na Wolfsburg ambazo zilichezwa mida ya saa mbili kasorobo.
Beki Gerald Pique alisaidia Barcelona kupata ushindi wa 1-0 dhidi ya wageni wao Dynamo Kyiv huku Salzburg ikipata ushindi wa 3-1 dhidi ya Wolfsburg.
Jumla ya mechi sita zilichezwa mida ya saa nne usiku.
Mechi ya kusisimua zaidi ilikuwa kati ya washindi wa kombe la Europa mwaka wa 2017 Manchester United na Atlanta ya Italia.
United ililazimika kutoka nyuma ili kupata ushindi baada ya kufungwa mabao mawili bila jawabu katika kipindi cha kwanza cha mechi hiyo ambayo ilichezewa ugani Old Trafford.
Mashetani wekundu walinoa makali yao baada ya kuenda kipindi cha mapumziko na wakarudi wakiwa na nguvu zaidi za kuwabwaga chini wageni wao. Mabao ya Marcus Rashford, Harry Maguire na Christiano Ronaldo yalisaidia United kupata ushindi wa kushtukiza katika kipindi cha pili.
Chelsea ilicheza dhidi ya Malmo FF ya Uswidi ugani Stamford Bridge na kupata ushindi mkubwa wa 4-0.Jorginho alifunga mikwaju miwili ya penalti huku Andreas Christensen na Kai Havertz wakifunga mabao hayo mengine mawili.
Bayern Munich pia walipata ushindi wa 4-0 ugenini dhidi ya Benfica. Mabao mawili ya Leroy Sane, moja la Robert Lewandowski na lingine la kujifunga yalisaidia Bayern kuwika ugenini.
Juventus walipata ushindi wa 1-0 ugenini dhidi ya Zenit St Petersburg, Washindi wa Europa League msimu uliopita Vilarreal wakashinda Young Boys 4-1 ugenini huku mechi kati ya Lille na Sevilla ikiishia sare ya 0-0.
Kwa sasa PSG inaongoza kundi A, Liverpool wako kileleni katika kundi B, Ajax wanaongoza kundi C, Sherrif Tiraspol kundi D, Bayern kundi E, Manchester United wako kileleni katika kundi F, Kundi G linaongozwa na Salzburg huku Juventus ikitawala kundi H baada ya mechi tatu.
Sebastian Haller wa Ajax, Robert Lewandowski wa Bayern na Mohammed Sala wa Liverpool wanaongoza kwa ufungaji mabao na mabao 6, 5 na 5 mtawalia.