Lukaku Kurejea Inter Kwa Mkopo Kutoka Chelsea

Kurudi kwake kulifanywa rasmi katika video

Muhtasari

•Klabu hiyo ya London ilitoa taarifa kuthibitisha "uhamisho wa mkopo wa msimu mzima".

Mshambuliaji wa Chelsea Romelu Lukaku
Mshambuliaji wa Chelsea Romelu Lukaku
Image: HISANI

Romelu Lukaku alirejea Inter Milan siku ya Jumatano baada ya kukamilisha uhamisho wa mkopo wa msimu mzima kutoka Chelsea mwaka mmoja tu baada ya uhamisho wake wa kulipwa kutoka Italia kwenda klabu hiyo ya Ligi Kuu ya Uingereza.

Mshambulizi wa Ubelgiji Lukaku ataungana tena na mashabiki wake wa zamani huko San Siro baada ya Chelsea kukubaliana na mkataba ambao Inter italipa pauni milioni nane za awali pamoja na marupurupu milioni tatu kwa mkopo huo.

Klabu hiyo ya London ilitoa taarifa kuthibitisha "uhamisho wa mkopo wa msimu mzima".

Kurudi kwake kulifanywa rasmi katika video iliyowekwa kwenye mitandao ya kijamii ya Inter huku Lukaku akisema  'we're back baby' (tumerudi)  alipokuwa akizungumza na mwenyekiti Steven Zhang juu ya paa la makao makuu ya klabu hiyo.

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 29 ataongoza tena safu ya ushambuliaji ya Inter wakati wakijaribu kurejesha taji la Serie A baada ya kuripotiwa kukatwa mshahara hadi pauni milioni 8.5 kwa kampeni ijayo.

Vyombo vya habari vya Italia viliripoti kuwa Inter na Chelsea wana makubaliano ya kiungwana kwamba mkopo huo unaweza kuongezwa kwa msimu mwingine iwapo uhamisho huo utafanikiwa.

"Inter imenipa mengi na ninatumai kuwa kuanzia sasa ninaweza kufanya vizuri zaidi kuliko hapo awali'' Lukaku alisema.