Michezo ya shule - Misikhu Kuwakilisha kanda yab Magharibi katika magongo

Mashindano ya kitaifa yatang’oa nanga mnamo tarehe 8 hadi 13 Septemba

Muhtasari

• Jimbo la Bungoma linajivunia shule ya upili ya wasichana ya mtakatifu Cecilia Misikhu, ambayo itawakilisha jimbo hilo katika ngazi ya kitaifa

Mchezaji wa Sshule ya Misikhu (jezi la samawati) akiwania mpira dhidi ya mwenzake wa Tigoi katika fainali ya michezo ya shule upili ya kanda ya Magaribi katika uga wa michezo wa Mumias.
Mchezaji wa Sshule ya Misikhu (jezi la samawati) akiwania mpira dhidi ya mwenzake wa Tigoi katika fainali ya michezo ya shule upili ya kanda ya Magaribi katika uga wa michezo wa Mumias.
Image: KNA

Baada ya kukamilika kwa michezo ya shule za upili za kanda, macho yote sasa yanaelekezwa kwenye ukanda wa kitaifa utakaong’oa nanga mnamo Alhamisi tarehe nane Septemba mwakani.

Jimbo la Bungoma linajivunia shule ya upili ya wasichana ya mtakatifu Cecilia Misikhu, ambayo itawakilisha jimbo hilo katika ngazi ya kitaifa kwenye mchezo wa magongo almaarufu Hockey.

Meza ya michezo ya KNA imefwatilia mitanange hio tangia ilipong’oa nanga katika ngazi ya zoni hadi kufikia upeo wa maeneo ambao ni mikoa. 

Shule hio ya upili ya mtakatifu Cecilia amekuwa na safari ndefu iliyojaa mishemishe na hamkani lakini tajiriba ya kikosi hicho iliwapa kipaumbele katika kipute hicho.

Mkufunzi wa kikosi cha Magongo shule ya upili ya Misikhu, Robert Kanga aliwamiminia sifa mabinti hao kwa kuonyesha ukakamavu na ushujaa wa aina yake. 

“Nawapongeza wasichana wetu kwa kupevuka kimtazamo na kimchezo kwani fainali ilikuwa dhidi ya bingwa wa kanda ya Magharibi,”  alisema.

Katika fainali ya mkoa, kikosi cha Misikhu kiliwalaza mabinti wa Tigoi mabao matatu kwa moja katika uga wa michezo wa Mumias. “Mazoezi na kujiamini ndiko kumetupa ushindi huu,” nahodha wa kikosi hicho Esther Juma Alisema.

Kikosi hicho cha Misikhu ambacho pia ndicho bingwa mtetezi wa ubingwa wa kitaifa wa magongo kimetinga tena kwa makali hata zaidi baada ya kukisuka kikosi chao upya wakiwa wamewapoteza wanangarambe wawili waliojiunga na vyuo vikuu.

“Kikosi changu kiko imara sasa na najivunia nahodha wangu Esther Juma ambaye amenifaa pakubwa katika maandalizi ya kipute cha kitaifa hapo Alhamisi,” mkufunzi Kanga alisema.

Kwa mujibu wa katibu mkuu wa shirikisho la michezo ya shule za upili Kenya Secondary Schools Association (KSSSA) David Ngugi, kipute hicho cha kitaifa kitang’oa nanga mnamo tarehe 8 hadi 13 Septemba huku washindi wakielekea moja kwa moja hadi mashindano ya jumuiya ya Afrika Mashariki baina ya tarehe 14 na 24 Septemba.

Kikosi cha Misikhu kimejumuishwa katika kundi A pamoja na shule ya upili ya Mwiki kutokea jimbo la Nairobi, shule ya wasichana ya Moi ya Marsabit kutokea eneo la Mashariki pamoja na ile ya mtakatifu Maria ya Taachasis kutokea Bonde la Ufa.

Kundi B la mashindano hayo kwa wasichana linawakutanisha shule ya wasichana ya Karima kutokea kati mwa nchi, ile ya Matuga kutokea Pwani, shule ya Transnzoia mixed ya Bonde la Ufa na ile ya Nyamira kutoka eneo la Nyanza.

Jimbo la Bungoma pia linajivunia uwakilishwaji katika   Hockey upande wa wavulana, kandanda ya wavulana na voliboli ya wavulana.

Shule ya upili ya Kamusinga itawakilisha jimbo hilo katika michuano ya magongo kwa wavulana huku shule ya upili ya wavulana ya Bukembe ikiiwakilisha Bungoma katika soka ya wavulana nayo ile ya wavulana ya Namwela ikijisatiti katika kipute cha voliboli.