Kocha wa timu ya Tusker inayoshiriki ligi kuu nchini Kenya Robert Matano amemchukulia hatua za kisheria mwenzake wa AFC Leopards Mbelgiji Patrick Aussems kwa kile alisema kuwa ni kumchafulia jina kwa kauli kuwa Matano anatumia uchawi na ushirikina kushinda mechi zake.
Katika barua ambayo imeonekana mitandaoni, mawakili wa Matano wamemuandikia Aussems, wanamkumbusha kuwa mnamo Aprili 9 baada ya mechi baina ya timu hizo mbili, Mbelgiji huyo alitamka maneno yanayoashiria kwamba Matano alitumia uchawi kushinda mechi hiyo.
“Kwa bahati mbaya tumeadhibiwa dakika za mwisho kwa kukosa ukali langoni mwa wapinzani. Hongera sana kwa wachezaji wa Tusker. Lakini mimi siko hapa kuzungumzia kuhusu kocha mzee ambaye hana uzoefu katika soka la ughaibuni na ambaye ako Zaidi katika kutumia djudju kuliko ufundi uwanjani,” Aussems aliwaambia wanahabari baada ya mechi hiyo.
Kufuatia maneno hayo, mawakili wa Matano walimkumbusha Aussems kuwa ni ya kumchafulia jina mteja wao na hatua za kisheria imebidi zichukuliwe.
“Kufuatia tamko lako hilo, mteja wetu amechafuliwa jina katika taaluma yake kama kocha mwenye uzoefu. Na heshima yake imepungua machoni mwa watu wenye fikira nzuri katika jamii na amepata aibu. Kwa hivyo tunakutaka utoe tamko la kuomba radhi na pia uchapishe msamaha huo kwenye Twitter ndani ya siku tatu, la sivyo tutachukua hatua mbadala,” sehemu ya barua ya mawakili wa Matano ilisoma.
Awali katika mahojiano na kituo kimoja cha redio, Matano alisema kuwa hangemuacha Aussems kuponyoka na maneno yake kuwa anatumia uchawi.
"Sitaacha chochote na kwa kuwa aliniahidi pambano mjini, niko tayari kwa ajili yake. Kitu ambacho sitamruhusu kuondoka nacho ni madai yake kwamba natumia uchawi kushinda mechi. Huyo hana budi kumthibitisha kuzimu, mbinguni, au duniani. Inabidi na lazima nipate jibu. Mimi ni Mkenya na kwa sababu yeye ni mgeni, anafikiri kwamba anaweza kuja hapa na kuzungumza takataka kunihusu nyumbani,” Matano alisema.