Mshambulizi matata wa PSG, Kylian Mbappe, yuko nchini Cameroon.
Nahodha huyo wa timu ya taifa ya Ufaransa aliwasili katika jiji kuu nchi hiyo ya Afrika Magharibi, Yaounde siku ya Alhamisi akiwa ameandamana na baba yake Wilfred Mbappe ambaye alizaliwa katika jiji kubwa la Douala.
Wawili hao walifika uwanja wa ndege jijini Yaounde na kupokelewa na mashabiki na maafisa wa soka nchini humo.
Ni ziara ya kwanza kwa Mbappe nchini humo tangu kuwa nyota wa kimataifa.
Katika ziara hiyo yake ya siku tatu, anatazamiwa kucheza mechi dhidi ya timu ya daraja la pili inayomilikiwa na mchezaji nyota wa zamani wa tenisi, Yannick Noah.
Mbappe pia atatumia siku chache zijazo kuzuru nchi hiyo, ambapo atakutana na wanahabari pamoja na kushirikisha mamlaka katika msururu wa shughuli.
Mkameruni huyo mzaliwa wa Ufaransa anatazamiwa kujenga kituo cha burudani na vituo vya kijamii nchini Cameroon.