Mchezaji kandanda wa kimataifa wa Ufaransa Kylian Mbappe anaendelea na ziara yake nchini Cameroon, Afrika Magharibi.
Picha na video za kustaajabisha za mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 24 anayechezea klabu ya Paris Saint Garmain ya Ufaransa almaarufu PSG akikaribishwa vyema katika nchi hiyo alikozaliwa baba yake zimekuwa zikiwasisimua mashabiki wa soka kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii.
Siku ya Jumamosi, babake mchezaji huyo, Wilfred Mbappe alimpeleka katika kijiji cha Jebale, eneo la Douala ambako alizaliwa. Wawili hao walikuwa wamelindwa vikali na walinzi na wanajeshi walipokuwa wakiwasili nyumbani.
Video zilizorekodiwa wakati wa kuwasili kwao jijini Douala zinaonyesha msafara wa magari ya kifahari yakimwongoza mchezaji huyo na baba yake kuelekea walikokuwa wakienda. Walinzi waliokuwa wamevalia suti nyeusi walionekana wakikimbia kando ya magari yaliyokuwa yakimsindikiza nyota huyo wa PSG.
Lori la kijeshi la kivita pia lilikuwa sehemu ya msafara huo.
Nahodha huyo wa timu ya taifa ya Ufaransa aliwasili katika jiji kuu nchi hiyo ya Afrika Magharibi, Yaounde siku ya Alhamisi akiwa ameandamana na baba yake Wilfred Mbappe ambaye alizaliwa katika jiji kubwa la Douala.
Wawili hao walifika uwanja wa ndege jijini Yaounde na kupokelewa na mashabiki na maafisa wa soka nchini humo.
Ni ziara ya kwanza kwa Mbappe nchini humo tangu kuwa nyota wa kimataifa.
Wakati akizungumza na waandishi wa habari Ijumaa, Mbappé alisema "anaheshimika" kuzuru Cameroon, nchi yake "ya asili".
"Nina furaha sana kuwa hapa," aliongeza, akisema kwamba watu wamemwonyesha "mapenzi" mengi.
Mshambuliaji huyo wa PSG ambaye alizaliwa Paris, Ufaransa, kwa baba Mcameroon na mama kutoka Algeria- pia alikutana na Waziri Mkuu wa nchi hiyo Joseph Ngute siku ya Ijumaa, pamoja na maafisa wengine.