Mshambulizi wa Liverpool na supastaa wa Soka wa Misri, Mohamed Salah ameripotiwa kutoa mchango kwa watu wa Gaza kupitia Egyptian Red Crescent, Mkurugenzi Mtendaji wa shirika hilo Rami al-Nazer amethibitisha kwa mujibu wa jarida la Egyptian Independet.
"Ni kweli, Mohamed Salah alitoa mchango kwa Hilali Nyekundu kusaidia watu walioathiriwa na shambulio la bomu la Israeli huko Gaza," Nazer aliiambia Youm7.
Nazer alikataa kufichua thamani ya mchango wa Salah, kulingana na matakwa ya mchezaji, akieleza: "Maelezo ya wafadhili au maelezo ya kile kilichotokea hayawezi kufichuliwa."
Lakini kwa mujibu wa taarifa za ndani ambazo hajijathibitishwa, inaarifiwa mchezaji huyo alitoa mchango wa dola milioni moja na nusu sawa na shilingi za Kenya milioni 225.
"Mohamed Salah ni nyota wa Misri ambaye ana idadi kubwa ya mashabiki na anaingiliana na masuala ya Kiarabu vyema," alisema.
Nazer alimsifu Salah, akisema ni mara ya kwanza kwa nyota huyo wa Misri kutoa mchango kwa Hilali Nyekundu.
Hatua ya Salah kutoa mchango kwa ajili ya ndugu Waislamu inakuja wakati ambapo mataifa mengi ya Ulaya yameonesha kusimama na Israel katika mzozo huo, huku wachezaji wengi wa Kiislamu wakizuiliwa kutoa matamshi yoyote ya kuonesha kusimama na Wapalestina ambao ni Waislamu wenzao.
Jeshi la Israel tarehe 7 Oktoba lilitangaza kuwa Israel ilikuwa katika ‘hali ya vita’ baada ya wanamgambo wa Hamas kurusha makombora na kutuma vikosi katika ardhi ya Israel.
"Ikiwa una bunduki, iondoe. Huu ndio wakati wa kuutumia - toka nje na malori, magari, shoka, leo historia bora na yenye heshima zaidi inaanza," kamanda wa kijeshi wa Hamas Muhammad Al-Deif alisema katika ujumbe uliorekodiwa kama ilivyoripotiwa na CNN.
Operesheni ya "Al-Aqsa Storm" ilikuwa mfululizo wa mashambulizi yaliyoratibiwa na makundi ya Wapalestina katika Ukanda wa Gaza na Israel siku ya Jumamosi.