Mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika 2024 (AFCON) yanayoendelea nchini Ivory Coast yaliingia siku ya tatu mnamo Jumatatu, Januari 15, huku mechi tatu zikichezwa.
Mechi ya kwanza kati ya mabingwa watetezi Senegal na Gambia ilichezwa mwendo wa saa kumi na moja jioni huku vijana wa Aliou Cisse wakiondoka na pointi zote tatu baada ya kushinda 3-0.
Mshambulizi wa Marseille, Pape Gueye alianza kufunga katika dakika ya 4 ya mechi hiyo kabla ya Gambia kupoteza mmoja wa wachezaji wake, Ebou Adams, kutokana na kadi nyekundu katika dakika ya 45+7. Kipindi cha kwanza kilimalizika 1-0 kabla ya Senegal kurejea kipindi cha pili na kumaliza kile ilichokianza.
Katika dakika ya 52, kiungo wa klabu ya Metz, Lamine Camara aliifungia Senegal bao la pili kabla ya kufunga lingine katika dakika ya 86.
Mechi ya pili ilikuwa kati ya Cameroon na Guinea na ilimalizika kwa sare ya 1-1.
Guinea walipata bao la kwanza katika dakika ya 10 kupitia kwa mshambuliaji Mohamed Bayo kabla ya kupunguzwa kwa bahati mbaya hadi wachezaji kumi kufuatia nahodha Francois Kamano kupewa kadi nyekundu katika dakika ya 45+2.
Cameroon baadaye walisawazisha katika dakika ya 51 kupitia kwa mshambuliaji Frank Magri.
Mechi ya mwisho kati ya Algeria na Angola ilichezwa mwendo wa saa tano usiku na pia ilimalizika kwa sare ya 1-1.
Baghdad Bounedjah wa Al-Sadd alianza kuifungia Algeria katika dakika ya 18 huku Mabululu akiifungia Gambia kwa penalti dakika ya 68.
Mechi zingine tatu zitachezwa siku ya Jumanne jioni kuadhimisha siku ya 4 ya michuano hiyo. Tazama mechi ya Jumanne;-
KUNDI D: Burkina Faso vs Mauritania (Saa kumi na jioni moja masaa ya Afrika Mashariki, Uwanja wa Stade de la Paix)
KUNDI E: Tunisia vs Namibia (Saa mbili usiku masaa ya Afrika Mashariki, Uwanja wa Amadou Gon Coulibaly)
KUNDI E: Mali vs Afrika Kusini (Saa tano usiku masaa ya Afrika Mashariki, Uwanja wa Amadou Gon Coulibaly)