Mshambulizi wa Bayern Munich na Uingereza, Harry Kane amesisitiza kuwa England inastahili kutwaa ubingwa wa kombe la taifa bingwa Ulaya almaarufu kama Euro.
Uingereza imepigiwa upatu kuwa miongoni mwa timu zenye uwezekano kwa asilimia kubwa kushinda taji hilo.Taifa hilo limeshinda taji kuu mara ya mwisho, 1966,kombe la dunia.
Kane amekuwa sehemu ya kikosi cha England kilichotinga fainali ya michuano ya Euro iliyopita, nusu fainali ya kombe la dunia 2018 na nane bora ya kombe la dunia mwaka 2022.
Kwenye mahojiano na Uefa kuhusu England kuwa miongoni mwa timu za kupigiwa upatu kushinda Euro;Nahodha Kane alijibu:
"Nadhani tumepata hadhi hii kupitia michuano yetu hadi sasa...lakini sisi pia ni timu ambayo haijawahi kushinda Euro, hivyo tunajaribu kuweka historia hapa. Ni lengo tunalotaka kufikia, lakini tunajua itakuwa njia ndefu na ngumu. Lazima tuhakikishe tunafanya kila kitu sawa kwa sababu ikiwa hauko kwa asilimia 100 kwenye mashindano haya, unaweza kuadhibiwa..."
Vile vile,Kane amekitaja kikosi cha England kama miongoni mwa vikosi bora kwenye mashindano hayo
"Kikosi hiki ni mojawapo ya bora zaidi, kama si bora zaidi, tumewahi kuwa nayo ukiangalia fomu na ligi husika ambazo wengi wetu tumecheza. Tuna vipaji vya ajabu vya vijana ambao hawana woga na wanataka tu kucheza na kushinda."
Mchezaji huyo pia anahisi kuwa mashindano hayo kufanyiwa Ujerumani,kumemfanya ahisi kuwa na utulivu na kujiskia nyumbani,kwani klabu yake ya Bayern Munich inashiriki kwenye ligi kuu ya Ujerumani.
Kuhusu jukumu lake kama nahodha, Kane alisema kuwa ni fursa anayojivunia na anatumai wachezaji wenzake watapata motisha kupitia kwake,kutokana na uzoefu wake.
"Kuiongoza England na kuwaongoza wavulana pengine ni fursa kubwa zaidi ninayoweza kuwa nayo kama mchezaji na kamwe sitaichukulia kuwa rahisi. Hisia hii ni ya kipekee kabisa. Ni heshima kufanya hivi kwa mara ya nne..."