Kocha wa Argentina, Lionel Scaloni, amesema kuwa bado anashuku iwapo nahodha wa timu yake, Lionel Messi, atacheza kwenye mechi ya robo fainali dhidi ya Ecuador mnamo Alhamisi kwenye uga wa NRG kufuatia kuumia kwenye misuli ya paja.
Messi, ambaye aliumiza misuli ya paja la kulia dhidi ya Chile, hakucheza mechi ya fainali ya kundi dhidi ya Peru. Kocha Scaloni, vilevile, alikosa mechi hiyo kufuatia kupata marufuku ya kutohudhuria mechi moja na CONMEBOL.
CHIO“Tutangoja masaa machache ndipo tufanye uamuzi. Siku nyingine huwa bora. Tutaamua kulingana na ujumbe tutakaopata leo,” Scaloni aliambia vyombo vya habari baada ya Messi kuonekana akiwa mazoezini na timu.
“Tutajaribu iwezekanavyo ili acheze na iwapo hawezi, tutatafuta suluhisho jingine kwa timu. Naenda kuzungumza naye leo na nadhani itakuwa bora achukue muda wake afanye mazoezi kadri awezavyo.”
Mabingwa watetezi Argentina wanatumai kushinda taji lao la 16 la Copa America. Watamenyana na timu ya umahiri, Ecuador, ambao walinyakua nafasi yao kwenye robo fainali baada ya kumaliza nafasi ya pili kwenye kundi B. Ecuador walinyakua nafasi hiyo baada ya kutoka sare ya 0-0 na Mexico.
“Ecuador ni kikosi kizuri kwa kuwa wana wachezaji bora na kocha bora. Ni miongoni mwa timu bora kwenye Copa America. Wana nafasi nzuri ya kuwania kwenye ubingwa wa taji,” Scaloni alisema.
Mbali na hayo, Scaloni aliongezea kuwa maonyesho hayo ya bara yalikuwa yamethibitisha kuwa mashindano bora ya kiwango cha juu kwani hamkuwa na upendeleo kwa atakayeshinda taji.
“Yeyote anaweza fika fainali kwa urahisi na kushindana na walio bora ulimwenguni. Kwenye michezo ya jana kati ya Colombia na Brazil, mchezo huo ulikuwa wa hali ya juu. Uruguay, vilevile, wanafanya vyema na si jambo la kushtua,” alisema.