Mabingwa wa ligi kuu ya FKF, Gor Mahia walipokea kichapo cha 1-0 mikononi mwa Red Arrows FC kutoka Zambia kwenye mechi ya ufunguzi ya kombe la Cecafa Kagame Cup.
Licha ya kuonyesha matumaini katika mchuano huo,mabingwa mara ishirini na moja wa ligi kuu ya FKF ,waliambulia patupu kwenye mchezo wa ufunguzi wa Kundi B uliochezwa kwenye uwanja wa Azam Complex jijini Dar es Salaam Jumatano usiku.
Kwenye mazungumzo na wanahabari baada ya mechi,kocha wa Gor Mahia Leonardo Martins Neiva amesema kuwa hana wasiwasi na anahisi ilikuwa ni kwa wachezaji wake bado kujifunza anachotaka kutoka kwake, jambo ambalo anaamini litarekebishwa na wakati.
"Mchezo mgumu kwa timu zote mbili, katika kipindi cha kwanza timu kutoka Zambia ilidhibiti mchezo katika dakika 25 za kwanza lakini baada ya hapo, tulirekebisha mambo machache na kupata uwiano lakini kwa ujumla, walicheza vizuri zaidi yetu," Neiva alisema .
Aliongeza; “Wakati wa mapumziko, tulirekebisha baadhi ya vitu na tuliporudi, tulikuwa na mpira na mzunguko lakini ni mchezo wa kwanza kwangu, hawanijui, hivyo tunahitaji muda zaidi kuweka pamoja masuala yetu ya kiufundi na kimwili.
Gor itakuwa inajaribu kufufuwa matumaini yao kwenye mechi ijayo dhidi ya Telkom Fc kutoka Djibouti kabla ya kumaliza mechi ya makundi dhidi ya Al Hilal.
Kwa sasa Al Hilal inaongoza kundi B kwa alama tatu,sawia na Red Arrows FC japo wana wingi wa mabao.