Ulinzi Stars imetangaza kuachana na kocha mkuu Anthony Kimani baada ya kuwafundisha kwa msimu mmoja pekee.
Katika kutangaza mabadiliko hayo, uongozi wa klabu ulimshukuru Kimani kwa uongozi wake wakati alipokuwa klabuni hapo.
“Tmu ya Ulinzi inapenda kutoa shukurani zake kwa Anthony Kimani kwa michango yake katika klabu wakati akiwa kocha mkuu.”
“Anthony Kimani atakuwa sehemu ya familia ya Ulinzi daima," ilisema taarifa ya klabu.
Kimani alitoa shukrani zake kwa kila mtu anayehusishwa na klabu hiyo.
"Nataka kuchukua fursa na kutoa shukrani zangu za dhati na pongezi kwa kila mmoja wenu.”
“Msimu huu uliopita umekuwa safari ya ajabu, iliyojaa changamoto, ushindi, na kumbukumbu nyingi ambazo nitahifadhi milele, "alisema.
"Wakati muda wangu hapa umekuwa mfupi, unganisho na uzoefu ambao tumeshiriki utakaa nami kila wakati.”
“Ninaamini katika uwezo wa timu hii na nina imani kuwa mambo makubwa yanawangoja nyinyi nyote.”
“Nawatakia nyote mafanikio na furaha tele, ndani na nje ya uwanja. Kwa shukrani nyingi na salamu za joto, "aliongeza.
Kimani alianza kuwa kocha mkuu na timu hio kabla ya kuanza kwa msimu uliopita na alikumbana na changamoto nyingi.
Timu hiyo ilijihakikishia usalama wao wa kusalia katika ligi ya FKF katika siku ya mwisho ya msimu kwa ushindi wa dhidi Kariobangi Sharks.
Kocha Kimani ni mchezaji wa zamani wa kimataifa wa Kenya ambaye alianza maisha yake ya ukocha katika AFC Leopards akiwa kocha msaidizi wa pili baada ya kuzichezea Mathare United na AFC Leopards.