Wanariadha wa Kenya Judith Jerubet na Daniel Muindi wamepigwa marufuku ya miaka miwili na mitatu mtawalia baada ya kupatikana na hatia ya kutumia dawa ya kusisimua misuli.
Judith Jerubet ni mshindi wa nishani ya shaba katika mbio za Wuhan Marathon 2024.Mjini Wuhan, Jerubet alikimbia 2:27:38 Machi 24, akimaliza nyuma ya Mare Dibaba wa Ethiopia (2:25:12) na mkenya mwenzake Pauline Chemning Korikwiang (2:26:40).
Taarifa iliyochapishwa na shirika la riadha la dunia la kupambana na utumiaji wa dawa za kusimumua misuli, inaonyesha kuwa, Jerubet alipatikana kwa kutumia dawa aina ya 'triamcinolone acetonide' iliyopigwa marufuku baada ya sampuli ya mkojo kufanyika huku akipigwa marufuku ya miaka miwili.
Jerubet aliwasilisha sampuli ya mkojo Machi 24,2024 huku maabara ya Beijing ikithibitisha kuwepo kwa dawa aina ya 'triamcionolone acetonide' Aprili 18,2024.
Muindi,mwenye umri wa miaka 29,mshindi wa medali ya fedha katika mbio za Lima Marathon za 2024, amezuiliwa pia kwa miaka mitatu baada ya sampuli ya mkojo iliyokusanywa katika mbio za Lima Marathon nchini Peru mnamo Mei 19 kugunduliwa kuwa na dawa iliyopigwa marufuku ya 'anabolic steroid norandrosterone'.
Wanariadha wote wawili wanakabiliwa na marufuku haya kama sehemu ya msako wa kitengo cha uadilifu wa riadha dhidi ya dawa za kusisimua misuli huku Kenya ikisalia kuwa mojawapo wa mataifa ambayo yanamulikwa kwa sana.