Klabu ya soka ya Manchester United imetangaza kumsajili beki chipukizi wa Ufaransa ,Leny Yoro, kutoka Lille OSC.
Katika taarifa yake ya Alhamisi jioni, klabu hiyo ya Ligi Kuu ya Uingereza ilitangaza kuwa beki huyo mwenye umri wa miaka 18 amesaini nao mkataba wa miaka mitano.
Klabu hiyo ilipongeza mafanikio ya Yoro hadi sasa na kuelezea matumaini yao makubwa naye.
"Manchester United inafuraha kuthibitisha kwamba Leny Yoro amejiunga na klabu, baada ya usajili. Beki huyo wa Ufaransa ametia saini kandarasi hadi Juni 2029, akiwa na chaguo la kuongeza mwaka mmoja zaidi,” ilisema taarifa ya Man United kwenye tovuti rasmi ya klabu.
Taarifa hiyo ilisomeka zaidi, “Akiwa na umri wa miaka 18 tu, Yoro tayari ameichezea Lille OSC mechi 60 za kikosi cha kwanza. Msimu uliopita, alitajwa katika timu bora ya Ligue 1 baada ya kuisaidia klabu yake kumaliza ligi ikiwa nafasi ya nne.”
Akizungumzia hatua hiyo, beki huyo chipukizi wa Ufaransa alisema kujiunga na Mashetani Wekundu ni hatua kubwa katika maisha yake ya soka na kueleza kuwa anafurahia jambo hilo.
"Kusaini kwa klabu yenye hadhi na matarajio ya Manchester United mapema sana katika maisha yangu ni heshima kubwa.
Tangu mazungumzo yangu ya kwanza na klabu, waliweka mpango wazi wa jinsi ninavyoweza kuendeleza Manchester kama sehemu ya mradi huu wa kusisimua, na walionyesha kujali sana kwangu na familia yangu. Ninajua kuhusu historia ya wachezaji wachanga katika Manchester United na ninahisi inaweza kuwa mahali pazuri pa kufikia uwezo wangu na kufikia matarajio yangu, pamoja na wachezaji wenzangu wapya. Siwezi kusubiri kuanza,” Yoro alisema.
Inaripotiwa kuwa klabu hiyo sasa imeelekeza macho yake kwa kiungo wa PSG, Manuel Ugarte, ambaye inasemekana wamekubaliana naye masuala ya kibinafsi.
Mchezaji huyo anadaiwa kutaka kuhamia klabu hiyo huku ikiendelea na mazungumzo na PSG.
Mashetani wekundu wako tayari kuwauza Casemiro na Scott McTominay ili kuongeza mabeki zaidi.