Klabu inayoshiriki ligi kuu ya Brazil, Fluminense ilifanikisha kuzuia kutofungwa kwa mara ya kwanza baada ya mechi 11.
Hii ni baada ya beki wa zamani wa Chelsea, Thiago Silva kuongoza safu ya ulinzi kwenye mechi yake ya kwanza na klabu hio.
Kwenye mechi 11 za awali walizokuwa wakicheza, Flumimense hawakuwa wameweka 'cleansheet' yoyote ile. Kwa sasa wanashikilia nafasi ya 19 kwenye jedwali mbele ya Atletico Go, wanaoburura mkia.
Ushindi wa Julai 21,2024 dhidi ya Cuiaba ulikuwa wa pili kwa klabu hio ya Brazil tangu Aprili 20,2024 kwenye ligi kuu ya Brazil ambapo waliwapiga Vasco da Gama 2-1 .
Silva alionyesha kufurahia baada ya mchezo huo huku akisema;
"Ni miaka 16 tangu nijawe na hisia nzuri kiasi hiki kuvaa jezi hii uwanjani. Bila shaka, huu ni muda ambao sitaweza kusahau na namshukuru Mungu kwa kuwa pamoja nami na kutusaidia kupata ushindi usiku huu." Silva alisema.
Silva alicheza kwa mara ya kwanza licha ya kujiunga na klabu hio mnamo Mei kwa kuwa dirisha la uhamisho nchini Brazil lilifunguliwa rasmi Julai 10.
Kifungu cha 10 cha kanuni mahususi za kitengo cha kwanza cha Brazil kinasema kwamba mchezaji mpya anaweza kuanza kushiriki mashindano siku moja baada ya jina lake kuchapishwa.
Silva ,39 aliondoka Chelsea Mei baada ya kandarasi yake kukamilika.Ameichezea klabu hiyo mara 152 na kusaidia kushinda kombe la klabu bingwa Ulaya mwaka 2021.