Michezo ya kwanza ya mashindano ya Olimpiki ya Paris ilichezwa siku ya Jumatano jioni katika mji mkuu wa Ufaransa.
Michuano hiyo ilianza rasmi kwa michezo ya raga ya wachezaji saba, ambapo mataifa kumi na mawili yaliwakilishwa, Kenya ikiwa miongoni mwa timu zilizoshiriki mashindano hayo.
Shujaa 7s hata hivyo hawakuweza kutamba katika mechi zao mbili za kwanza, ambapo walipoteza zote mbili kwa Argentina na Australia.
Vijana wa kocha Kelvin Wambua walipigwa 12-31 na Argentina na 7-21 na Australia katika mechi zilizochezwa mwendo wa saa kumi alasiri na saa mbili usiku mtawalia siku ya Jumatano.
Wamepangwa kumenyana na Samoa mwendo wa saa tisa alasiri siku ya Alhamisi katika mchezo wao wa mwisho wa hatua ya makundi.
Kwa sasa, Shujaa 7S wamekalia nafasi ya mwisho ya kundi B wakiwa na pointi mbili pekee huku Argentina na Australia zikishika nafasi za kwanza kwa pointi 6 kila moja.
Siku chache zilizopita, Kenya ilituma jumla ya wanariadha 81, makocha 43, wajumbe 5 wa kamati ya Olimpiki, wajumbe 26 wa timu ya usimamizi pamoja na wakuu watatu, hivyo ujumbe ukiwa jumla ya wanachama 161.
Kulingana na orodha hiyo, Katibu wa Kudumu katika wizara ya Michezo Peter Tum ndiye atakuwa mkuu wa wajumbe huku Dan Wanyama akiwakilisha Bunge la Kitaifa kama mkuu wa usimamizi wa michezo katika Kamati ya Bunge ya Michezo na Utamaduni ambapo yeye ndiye mwenyekiti.
Wakati huo huo, Julius Murgor anawakilisha Seneti kwa niaba ya Kamati ya Leba na Ustawi wa Jamii ambapo yeye ndiye mwenyekiti.
Kenya itawakilishwa katika michezo sita tofauti ambayo ni Riadha, Raga, Fencing, Voliboli, Judo na Kuogelea huku Riadha ikijumuisha Wanariadha wengi zaidi.
Michezo ya Olimpiki ya Paris 2024 itafunguliwa rasmi Ijumaa, Julai 26.