Wanariadha kutoka Kenya wanazidi kushamiri katika majukwaa ya kimataifa baada ya baadhi yao kuteuliwa kwenye orodha ya wanaowania tuzo ya mwanariadha bora wa mwaka katika mwaka wa 2024.
Tuzo hizo zinahusisha wanariadha wa kike na kiume kutoka duniani kote waliokimbia katika mashindano mbali mbali ya riadha.
Tuzo hizo zinazoandaliwa na shirikisho la riadha duniani, zinalenga kutambua wanariadha waliofanya vyema katika mashindano ya Olimpiki yaliyofanyika Paris, nchini Ufaransa.
Upande wa wanawake, Mkenya Faith Kipyegon ameteuliwa kuwania tuzo hizo baada ya kushinda mbio za mita 1,500 sawia na kuweka rekodi ya dunia katika mbio hizo.
Vilevile kwenye tuzo hizo hizo Mkenya Beatrice Chebet ameteuliwa baada ya kushinda mbio za mita 5,000 na 10,000 pamoja na kuandikisha rekodi mpya ya dunia kwa mbio za mita 10,000.
Upande wa wanaume, Emmanuel Wanyonyi ameteuliwa kwa tuzo hizo baada ya kushinda dhahabu kwenye mbio za mita 800 kwenye Olimpiki na Diamond League.
Wakenya hao wanatarajia ushindani mkubwa katika kura kutoka kwa wanariadha wengine ikiwemo Julien Alfred (Saint Lucia), Sydney McLaughlin(USA), Marileidy Paulino (Dominican Republic) na Gabby Thomas (USA) kwa upande wa wanawake.
Emmanuel Wanyonyi naye anatarajia ushindani mkubwa kutoka kwa Rai Benjamin, Grant Holloway na Noah Lyles wote wa USA pamoja na Letsile Tebogo wa Botswana.
Mchakato wa kupiga kura utakamilika tarehe 27.