(+Picha) Mwanariadha Hellen Obiri apandishwa cheo katika idara ya Jeshi la anga

Obiri alivishwa madaraka hayo na mkuu wa jeshi nchini jenerali Robert Kabochi katika ofisi zake siku ya Jumanne

Muhtasari

•Siku moja tu baada ya mshindi wa medali ya fedha kwenye mbio za mita 1500 Timothy Cheruiyot kupandishwa cheo kutoka kuwa mkaguzi mkuu wa mageraza na kufanywa msimamizi mwandamizi wa magereza, mwenzake wa kike Hellen Obiri  pia ameweza kupandishwa cheo.

Mkuu wa jeshi Robert Kabochi na mwanariadha Hellen Obiri wakati wa kuvishwa madaraka zaidi
Mkuu wa jeshi Robert Kabochi na mwanariadha Hellen Obiri wakati wa kuvishwa madaraka zaidi
Image: FACEBOOK// ROBERT KABOCHI

Serikali imeendelea kuwatunuku wanariadha wa Kenya ambao waliandikisha matokeo mazuri katika mashindano ya Olimpiki ambayo  yalifanyika jijini Tokyo, Japan.

Kando na zawadi ya pesa ambazo rais Uhuru Kenyatta aliwapatia wanariadha hao siku ya Jumatatu, baadhi yao sasa watafurahia madaraka zaidi katika vituo vyao vya kazi.

Siku moja tu baada ya mshindi wa medali ya fedha kwenye mbio za mita 1500 Timothy Cheruiyot kupandishwa cheo kutoka kuwa mkaguzi mkuu wa mageraza na kufanywa msimamizi mwandamizi wa magereza, mwenzake wa kike Hellen Obiri  pia ameweza kupandishwa cheo.

Obiri ambaye alishindia Kenya nishani ya fedha katika  mbio za mita 5000 upande wa wanadada na ambaye anafanya kazi na idara ya wanajeshi wa anga  amepokea madaraka zaidi kutoka kuwa sajenti na kufanywa  sajini mkuu.

Obiri alivishwa madaraka hayo na mkuu wa jeshi nchini jenerali Robert Kabochi katika ofisi zake siku ya Jumanne.

Kabochi aliwapongeza wanariadha wa KDF ambao waliwakilisha taifa katika mashindano ya Olimpiki na kuwashawishi kuendelea na mazoezi zaidi.

"Nawapongeza sana Ssgt Obiri na Sgt Kigen kwa kuwakilisha Keya na KDF katika mashindano ya kidunia. Hongera. Nawasihi muendelee kuwa na nidhamu na kufanya kazi kwa bidii katika kazi zenu. Pia nawaomba pamoja na wanariadha wengine wa KDF mtumie kituo cha mafunzo cha Ulinzi Sports Complex kilicho Langata kufanya mazoezi zaidi" Kabochi alisema kupitia mtandao wake wa Facebook. 

Mwanariadha Benjamin Kigen ambaye alijishindia nishani ya shaba katika mbio za mita  3000 kuruka viunzi pia alihudhuria hafla hiyo.