Mwanariadha Eliud Kipchoge azindua mradi utakaosaidia sekta ya elimu na utunzaji wa mazingira

Muhtasari

•Kipchoge amesema kuwa lengo lake kuu ni kuwezesha watoto kote duniani kupata elimu.

•Kipchoge ameomba watu wa nia njema kumsaidia kutimiza lengo lake.

Image: FACEBOOK// ELIUD KIPCHOGE

Mwanariadha tajika kote ulimwenguni Eliud Kipchoge amezindua mradi wa 'Eliud Kipchoge Foundation' ambao unatazamia  kusaidia katika sekta ya elimu na utunzaji wa mazingira.

Akitangaza hatua hiyo kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii, Kipchoge amesema kuwa lengo lake kuu ni kuwezesha watoto kote duniani kupata elimu.

Kipchoge amesema kwamba kupitia mradi huo ana matumaini ya kuchangia kwenye sekta ya elimu na utunzaji wa mazingira.

"Nina raha kuzindua 'Eliud Kipchoge Foundation' leo. Lengo langu ni kupatia watoto wote duniani  uwezo wa kupata elimu na mafunzo. Nataka watoto hao wakue kuwa watu wakubwa wenye afya katika mazingira safi ambapo vichaka vinaweka watu wetu katika hali salama.

Natumai kuchangia na kukuza sekta ya elimu na utunzaji wa mazingira kupitia mradi huu. Nifikie watu wote kupitia sauti yangu" Kipchoge amesema.

Kipchoge ameomba watu wa nia njema kumsaidia kutimiza lengo lake.