Kenya yang'aa katika mashindano ya Boston Marathon

Muhtasari

•Mwanariadha Benson Kipruto alinyakua nishani ya dhahabu kwenye mbio za wanaume baada ya kukimbia umbali wa kilomita 42  na masaa mawili, dakika 9 na sekunde 51.

•Kenya iling'aa zaidi kwenye mbio za wanawake kwani wanariadha wawakilishi waliweza kunyakua medali zote tatu.

Benson Kipruto
Benson Kipruto
Image: BOSTON MARATHON

Bendera ya Kenya ilipaa juu angani kwenye mashindano ya 125 ya mbio za Boston Marathon yaliyoandaliwa nchini Marekani siku ya Jumatatu baada ya wanariadha ambao waliwakilisha taifa kuonyesha umahiri wao na kuwabwaga chini wenzao kutoka mataifa mengine.

Mwanariadha Benson Kipruto alinyakua nishani ya dhahabu kwenye mbio za wanaume baada ya kukimbia umbali wa kilomita 42  na masaa mawili, dakika 9 na sekunde 51.

Lemi Berhanu kutoka Ethiopia aliibuka wa pili baada ya kukimbia kwa masaa mawili, dakika 10 na sekunde 37 huku mwenzake Jemal Yimer  akijishindia shaba baada ya kumaliza sekunde moja tu nyuma yake.

Kenya iling'aa zaidi katika mbio za wanawake kwani wanariadha wawakilishi waliweza kunyakua medali zote tatu.

Diana Kipyogei
Diana Kipyogei
Image: BOSTON MARATHON

Mwanariadha Diana Chemtai Kipyogei alishinda dhahabu baada ya kutumia masaa mawili, dakika 24 na sekunde 45 kumaliza mbio hizo.

Edna Kiplagat aliibuka wa pili baada ya kukimbia kwa masaa mawili dakika 45 na sekunde 9 huku Mary Ngugi akimfuata kwa karibu na masaa mawili dakika 25 na sekunde 20.

Nafasi ya nne pia ilichukuliwa na Mkenya Monicah Ngige.