Eliud Kipchoge, Faith Kipyegon wateuliwa kuwania tuzo za wanariadha bora mwaka wa 2021

Muhtasari

•Kipchoge alinyakua nishani ya dhahabu kwenye mbio za Marathon katika mashindano ya  2020 Tokyo Olympics ambayo yalifanyika mwezi Julai na Agosti mwakani.

•Kipyegon aliweza kumbwaga  mshindani wake wa karibu Sifan  Hassan na kunyakua dhahabu katika mbio za  mita 1500 huko Tokyo baada ya kumaliza kwa dakika tatu na sekunde 53.11.

Image: HISANI

Wanariadha wawili mahiri kutoka Kenya wameorodheshwa miongoni mwa wanariadha 20 ambao wameweza kung'aa zaidi duniani mwaka huu.

Shirika la riadha Ulimwenguni limemteua bingwa wa mbio za Marathon Eliud  Kipchoge kuwania tuzo la mwanariadha bora wa kiume mwaka wa 2021 huku nyota wa mbio za mita 1500 Faith Kipyegon akiteuliwa kuwania tuzo la mwanariadha bora wa kike mwaka wa 2021.

Kipchoge atamenyana na vigogo wengine wa riadha kama Joshua Cheptegei wa Uganda, Jacob Ingebrigtsen wa Norway, Pedro Pichardo wa Portugal, Karsten Warholm wa Norway, Daniel Stahl wa Sweden, Ryan Crouser wa Marekani, Damian Warner wa Canada, Miltiadis Tentoglou wa Ugiriki na Mondo Duplantis wa Uswidi.

Kwa upande wa wanawake Faith Kipyegon ameorodheshwa pamoja na mastaa wengine kama Sifan Hassan wa Uholanzi, Elaine Thompson-Herah wa Jamaica, Athing Mu wa Marekani, Valarie Allman wa Marekani, Shaunae Miller-Uibo wa Bahamas, Jasmine Camacho-Quinn wa  Puerto Rico, Yulimar Rojas wa Venezuela Mariya Lasitskene wa Urusi na Sydney Mclaughlin wa Marekani.

Kipchoge alinyakua nishani ya dhahabu kwenye mbio za Marathon katika mashindano ya  2020 Tokyo Olympics ambayo yalifanyika mwezi Julai na Agosti mwakani. Mwanariadha huyo aliweza kujishindia dhahabu yake ya pili kwenye mashindano ya Olympics baada ya kukamilisha mbio hizo kwa masaa mawili dakika nane na sekunde 38.

Kipyegon aliweza kumbwaga  mshindani wake wa karibu Sifan  Hassan na kunyakua dhahabu katika mbio za  mita 1500 huko Tokyo baada ya kumaliza kwa dakika tatu na sekunde 53.11.