Asbel Kiprop kurudi mbioni baada ya marufuku kukamilika

Muhtasari

• Mwaka wa 2018, vipimo vilionesha Asbel Kiprop alikuwa ametumia dawa za kutitimua missuli kinyume na kanuni za shirika la wanariadha duniani IAAF katika vipimo alivyofanyiwa na kitengo cha uadilifu cha riadha.

• Baada ya marufuku hiyo kukamilika, Kiprop amewashukuru wote waliosimama upande wa faraja yake wakati alikuwa anakaribia kukata tamaa katika riadha.

asbel kiprop
asbel kiprop

Mwanariadha wa mbio za mita 1500, Asbel Kiprop anatarajiwa kurejea kwenye ulingo baada ya marufuku aliyolimbikiziwa ya miaka minne kukamilika rasmi Februari 2.

Mwaka wa 2018, vipimo vilionesha Asbel Kiprop alikuwa ametumia dawa za kutitimua misuli kinyume na kanuni za shirikisho la riadha duniani IAAF katika vipimo alivyofanywa na kitengo cha uadilifu cha riadha.

Katika taarifa kutoka kwa wakili wake miezi miwili baada ya marufuku hiyo, Kiprop alidai kwamba vipimo hivyo vilikuwa vya uongo na vilivyokuwa vikilenga kumkata miguu.

“Ninasisitiza kwamba sikutumia dawa zilizopigwa marufuku dhidi ya wanariadha. Nitazidi kushikilia kauli yangu ya kutokuwa na hatia kwangu, hata kama inamaanisha sitoweza kushiriki katika riadha kwa miaka minne ijayo,” Kiprop aliteta.

Baada ya marufuku hiyo kukamilika, Kiprop amewashukuru wote waliosimama upande wa faraja yake wakati alikuwa anakaribia kukata tamaa katika riadha.

“Wakati miaka minne ya marufuku inakamilika rasmi, ningependa kumshukuru Mungu, familia yangu pamoja na mwajiri wangu NPS kwa usaidizi wa jumla na uelewa wa kina wakati nilikuwa nimetamauka kwa madai bandia ya kutumia dawa za kutitimua misuli,” Kiprop aliandika.

“Pia nisingependa hili lipite bila kushukuru vyombo vya Habari nchini Kenya kwa kunisikiliza na kunipa nafasi ya kujieleza nilipokuwa nalalamikia madai ya uwongo yaliyolimbikizwa kwangu. Ahsante sana,” Kiprop alisema.

Asbel Kiprop
Image: Facebook

Mwanariadha huyo ambaye pia ni polisi amesisitiza kwamba hana hatia inayomlazimu kuomba radhi kwa kuwa haikuwa makosa yake wala uzembe wake na kuongeza kuwa siku zote yeye amekuwa akitetea mchezo safi.

Amemaliza kwa kuwaahidi mashabiki wake kuwa anatarajia kurejea kwa uwazi na kwa maendeleo ya polepole ili kushinda mbio katika mashindano mbalimbali.