Aliyekuwa bingwa wa marathon Duncan Kibet 'Jamaica' asimulia masaibu yake maishani

Muhtasari

• Jamaica alikuwa ni mwanariadha wa kupigiwa mfano si tu katika mbio bali hata kwa jinsi alivyokuwa akijibeba kwa fasheni.

• Anasema hali yake iligeuka ghafla na utajiri kuyeyuka pindi alipopata jeraha na kutapeliwa mali zake, jambo lililompelekea kupoteza dira maishani mpaka sasa.

Duncan 'Jamaica' Kibet wakati wa mahojiano nyumbani kwake katika Kijiji cha Cheramei, Kaunti ya Uasin Gishu.
Image: EMMANUEL SABUNI

Safari ya Duncan ‘Jamaica’ Kibet ni moja ambayo itaacha hata watu wenye roho ngumu zaidi wakibubujikwa na machozi.

 

Ni mwanamume ambaye aliinuka kutoka maisha ya uchochole hadi mtu tajika na kuwa mmoja wa wanariadha wa mbio za marathoni wa Kenya. Alijizolea mamilioni ya pesa kabla ya kutazama utajiri wake ukiyeyuka kutokana na walaghai.

 

Kutokana na misukosuko hii, bingwa wa mbio za Rotterdam Marathon 2009 amekuwa akipambana na mfadhaiko na msongo wa mwazo na hata kujaribu la kujitoa uhai mara tatu ili kumaliza maumivu yake haraka.

Hali yake ni ya ufukara kiasi kwamba anathamini sana hata Shilingi 100 tu mfukoni mwake hivi sasa.

“Ikitokea sasa nikipata shilingi mia nitashukuru sana, sijui ni lini nitapata zingine, kitu kizuri ni kwamba nimekubali nipo chini na sinywi pombe. Ningekuwa mlevi, ningepotezwa sana," bingwa huyo wa 2004 wa Lille Half Marathon anasema.

 Kibet alikuwa mwanariadha wa pili kwa kasi kushinda Marathon ya Rotterdam kwa saa 2:04.27. Lakini taaluma yake nzuri iligonga mwamba baada ya kupata jeraha.

Kabla ya misururu ya masaibu kumjia na kumsababishia hali yake ya sasa, 'Jamaica' alikuwa mwanariadha mpevu na mwenye haiba katika mbio za masafa marefu -  alitambulika kwa ndevu zake zilizokolea na shingoni hungekosa mkufu wa bei   (bling bling)  shingoni mwake.

Duncan 'Jamaica' Kibet wakati wa Rotterdam Marathon
Image: Maktaba

Anakumbuka kwa uchungu kuhusu maisha ya furaha ya zamani. 

"Ningeweza kupata kila nilichotaka kwa sababu nilikuwa na pesa. Nilipenda kushindana na mikufu, ilikuwa kama sehemu ya mavazi yangu. Si jambo zuri kuwa maskini, sio hisia nzuri kuwa ombaomba, unaelewa?" aliguna Jamaica kwa maneno yenye majuto mengi. 

Ndoto yake ya utotoni kufika hatua ya kimataifa ilimsukuma kumfuata kaka yake mkubwa kwa mafunzo na mazoezi ya riadha kila asubuhi. 

"Mbali na kumuona kaka yangu akifanya mazoezi, pia nilitamani kusafiri kote ulimwenguni kwa ndege, nikishindana katika mbio kuu, kushinda na kuwa maarufu," bingwa wa 2009 wa Lagos Marathon anasema. 

Mnamo 2009, alishinda Amsterdam Marathon katika muda wa rekodi wa 2:04:56, na kumfanya kuwa mwanariadha wa pili mwenye kasi zaidi wa muda wote nyuma ya gwiji wa Ethiopia Haile Gebresellasie ambaye alikuwa mshikilizi wa rekodi ya dunia wakati huo kwa muda wa 2:03:59.

Akiwa na uchu, hamu na ari ya mafanikio zaidi, alianza mazoezi ya Berlin Marathon mwaka uliofuata. Jamaica aliendelea kujitayarisha kwa ajili ya mbio hizo, huku akipuuza maumivu madogo aliyokuwa akihisi. 

"Nilitoka nje nikiwa na umbali wa kilomita 30 kwa sababu maumivu hayakuvumilika. Nilirudi nyumbani nikiwa nimekata tamaa kidogo lakini nilijua bado nina nafasi ya kufanya vizuri zaidi. Tulianza matibabu lakini maumivu hayakuisha kwa sababu kulikuwa na msuli unaoitwa soleus na mchakato wa uponyaji ulikuwa wa polepole sana,” alikumbuka Jamaica. 

Jeraha hilo pia lilimsababishia mmomonyoko mfukoni ambapo alitumia kiasi kikubwa cha fedha kujihudumia. 

"Ningeweza kuanza kuwekeza mwaka 2010 kwa sababu taaluma yangu ya riadha ilikuwa inakaribia kilele, lakini sasa jeraha liliniweka nje kabisa. Huu sasa ni mwaka wa 10, sina chochote, sina chochote kabisa na huwezi amini,” baba wa watoto wawili anakumbuka kwa machungu.

Mnamo Februari 2012, akiwa na hamu ya kurejea kwenye ulingo wa riadha duniani, Jamaica aliingia katika makubaliano ya kubadilishana mali zake ili kupata pesa za kutibu jeraha lake. Kutokana na makubaliano hayo, alipokea Shilingi milioni 2, alizotumia kwenda kutibiwa Ujerumani na alitarajia kupokezwa zingine Shilingi milioni 3. 

"Nilipokea Shilingi milioni mbili na nikaenda Ujerumani kwa matibabu. Nikiwa huko kwa ajili ya matibabu, ningeuliza mara kwa mara iwapo hatimiliki ilikuwa imehifadhiwa kwa wakili wangu ili kurahisisha uhamisho wa umiliki huo kwangu lakini kila kitu kilionekana kujikokota. Hakuna kilichokuja kwa matakwa yangu," Jamaica anakariri.  

Haikupita muda akagundua kuwa alikuwa ametapeliwa.

"Nilipokea hati miliki hiyo mwaka wa 2015 tu lakini nikagundua kuwa nyumba hiyo ilikuwa imewekwa kama dhamana ya mkopo, ambapo sikujua chochote. Kisha nilifukuzwa kutoka kwa mali hiyo na kulazimika kurudi nyumbani kwa mama yangu," Jamaica alieleza kwa mfadhaiko. 

Bila makazi, senti na kazi, Kibet alirudi kwa nyumba ya mzazi wake kama njia moja ya kujaribu kutafuta amani lakini dhiki zake ziliendelea kumuandama. 

"Nilikuwa naamka saa tisa alfajiri kwa maombi. Nimejaribu kujiua mara tatu, kila ninapokumbuka mali yangu niliyotapeliwa," Jamaica alikiri. 

Kwa muda huo wote, jitihada zake za kupata haki zimeonekana kuwa bure. Sasa anatoa wito kwa serikali na wanariadha wenzake kusimama naye katika harakati zake za kutafuta haki. Pia ana matumaini ya kurejea katika mbio mara tu atakapotatua dhiki zake. 

"Nikipata haki kama sasa hivi, nitarudi katika hali yangu ya zamani. Nitaanza mazoezi. Najijua, nahisi jeraha limepona na bado naweza kukimbia. Pia nitarejea shuleni," anamalizia.