Wa kuvunja rekodi ya dunia ni mimi- Omanyala asema huku akijiandaa kwa fainali Mauritius

Muhtasari

•Omanyala alifuzu fainali ya Senior Africa Athletics Championships baada ya kuandikisha muda bora zaidi katika nusu fainali za kombe hilo. 

•Omanyala ameweka wazi kuwa lengo lake kuu ni kuvunja rekodi ya dunia ambayo kwa sasa inashikiliwa na Usian Bolt wa Jamaica.

Ferdinand Omanyala
Ferdinand Omanyala
Image: HISANI

Mwanariadha wa mbio za mita 100 Ferdinand Omanyala ameshikilia kuwa mawazo yake yote kwa sasa yapo kwenye fainali za Senior Africa Athletics Championships zitakazofanyika leo  (Juni 9)  jijini Reduit, Mauritius.

Omanyala ambaye ndiye anashikilia rekodi ya Kiafrika katika mbio za mita 100 alifuzu fainali ya Senior Africa Athletics Championships baada ya kuandikisha muda bora zaidi katika nusu fainali za kombe hilo. 

Mwanariadha huyo mwenye umri wa miaka 26 alikimbia kwa sekunde 10.07 huku Maseko Gilbert wa Namibia akiibuka wa pili kwa sekunde 10.15 na Noa Bibi wa Mauritius akiandikisha sekunde 10.24.

"Zilikuwa mbio nzuri...10.07 ni muda mzuri sana. Kwa hiyo sasa mawazo yangu yapo kwenye fainali, kwenye mstari wa mwisho kwa sababu unapoweka akili yako kwa washindani, utaishia kukimbia mbio zao," Omanyala alisema baada ya kufuzu kushiriki fainali.

Omanyala ameweka wazi kuwa lengo lake kuu ni kuvunja rekodi ya dunia ambayo kwa sasa inashikiliwa na Usian Bolt wa Jamaica.

Alivunja rekodi ya Afrika mwezi Septemba mwaka jana baada ya kumaliza mbio hizo kwa sekunde 9.77 wakati wa  Kip Keino Classic Tour .

"Rekodi ya dunia sio ya kipekee na hakuna lisilowezekana katika ulimwengu huu. Naamini itavunjwa na wa kuivunja ni mimi maana hakuna aliyeamini kuwa Mkenya anaweza kukimbia haraka," Omanyala alisema katika mahojiano na BBC.

Mwanariadha huyo alisema kuwa hakuwahi kufikiria angefikia hatua ambayo ameweza kufikia sasa.

Rekodi ya sasa ya dunia katika mbio za 100 ni sekunde 9.58 ambayo iliandikishwa na Usian Bolt katika mbio za IAAF World Championship mwaka wa 2009.