Hongera! Kenya yang'aa katika mbio za kupokezana vijiti za wanaume kwa wanawake

Kenya imetwaa dhahabu ya kwanza kwenye mashindano ya World Cross Country.

Muhtasari

•Emmanuel Wanyonyi, Mirriam Cherop, Kyumbe Munguti na Brenda Chebet waliipa timu ya Kenya ushindi.

•Wanne hao waliipa Kenya dhahabu ya kwanza katika shindano hilo la kimataifa lililoanza  leo, Februari 18 asubuhi.

wametwaa ushindi katika mbio za kupokezana ushindi za wanaume kwa wanawake
Wanariadha wa Kenya wametwaa ushindi katika mbio za kupokezana ushindi za wanaume kwa wanawake
Image: WORLD ATHLETICS

Kenya imeibuka mabingwa wapya wa Dunia katika mbio za kupokezana vijiti za jinsia zote kwenye mashindano ya World Cross Country yanazoendelea.

Emmanuel Wanyonyi, Mirriam Cherop, Kyumbe Munguti na Brenda Chebet waliipa timu ya Kenya ushindi katika mbio hizo za wanaume na wanawake zilizofanyika jijini Bathurst, Australia siku ya Jumamosi asubuhi.

Mwanariadha wa mbio za mita 800 Emmanuel Wanyonyi ndiye alianza kwa upande wa Timu Kenya kabla ya kukabidhi kijiti kwa mwenzake Miriam Cherop huku Kenya ikienda nyuma ya wenyeji Australia mwishoni mwa mzunguko wa nne. Daniel Munguti kisha alipokea kijiti na kumpita Stewart Mcsweyn wa Australia kabla ya kumkabidhi  Brenda Chebet ambaye alihakikisha Kenya imepata ushindi.

Wanariadha wa Kenya walitumia muda wa dakika 23 na sekunde 21 mbele ya timu ya Ethiopia ambayo iliibuka ya pili kwa dakika 23, sekunde 23 huku wenyeji Australia wakifanikiwa kutwaa shaba kwa dakika 23 na sekunde 26. Afrika Kusini, Marekani na Uingereza kisha zilifuata kwa mpangilio wa mfululizo.

Wanne hao waliipa Kenya medali ya kwanza ya dhahabu katika shindano hilo la kimataifa lililoanza  leo, Februari 18 asubuhi.