•Finot alisisimua mashabiki alipomkimbilia mpenzi wake na kumchumbia mara tu baada ya kushiriki fainali za wanawake za mita 3000 kuruka viunzi na maji.
•Finot pia alisema kwamba Bargiela kila mara alimpa nguvu-- ikiwa ni pamoja na wakati wa fainali za Jumanne.
Sio tu roho ya mashindani, lakini pia upendo umekuwa ukitanda hewani jijini Paris huku Michezo ya Olimpiki ikishuhudia matukio ya kupendeza ya mapenzi.
Mnamo Jumanne, Agosti 6, mwanariadha wa Ufaransa, Alice Finot alisisimua mashabiki wakati alipomkimbilia mpenzi wake na kumchumbia mara tu baada ya kushiriki fainali za wanawake za mita 3000 kuruka viunzi na maji.
Ingawa Finot hakushinda mbio hizo au medali yoyote, lakini aliweza kuvunja rekodi ya Uropa ya mbio za mita 3000 kuruka viunzi na maji kwa wanawake.
Mara tu baada ya kumaliza katika nafasi ya nne katika mbio hizo, mwanariadha huyo alipiga hatua muhimu sana kwa kumchumbia mpenzi wake wa muda mrefu, mwanariadha wa Uhispania Bruno Martínez Bargiela.
Katika video iliyosambaa mitandaoni, Finot alisimama kidogo kusherehekea hatua hiyo muhimu kabla ya kukimbia kwenye stendi ambapo Bargiela alikuwa amesimama - na kuushtua umati kwa kitendo cha kupendeza alichofanya.
Kisha alichomoa pini iliyokuwa na ujumbe na kupiga magoti kwa goti moja ili kumchumbia mpenzi wake huku umati ukiwashangilia wanandoa hao kwa muda huo.
Wakati akizungumza na waandishi wa habari baada ya mbio - na baada ya kumchumbia mpenziwe - Finot alithibitisha kwamba Bargiela alisema "ndio."
"Nilijiambia kwamba ikiwa ningekimbia chini ya dakika tisa, nikijua kwamba tisa ni nambari yangu ya bahati na kwamba tumekuwa pamoja kwa miaka tisa, basi ningechumbiana," alisema.
"Sipendi kufanya mambo kama kila mtu mwingine. Kwa kuwa alikuwa bado hajaifanya, nilijiambia kuwa labda ilikuwa juu yangu kuifanya. Kwa hiyo, nilitoa pini ambayo nilikimbia nayo kwa mpenzi wangu. Juu yake, inasema: Upendo uko Paris,” alisema.
Finot pia alisema kwamba Bargiela kila mara alimpa nguvu-- ikiwa ni pamoja na wakati wa fainali za Jumanne.
"Nilifurahi sana, niliweza kujieleza," alisema kuhusu tukio hilo.
Kuhusu kumaliza kwake katika nafasi ya nne, aliongeza, “Ilikuwa ni muda kidogo tu (hilo lilikosa) kupata medali, samahani. Lakini sijutii chochote.”
Akitumia muda wa 8:58.67, Finot aliibuka wa nne nyuma ya washindi Winfred Yavi wa Bahrain, Peruth Chemutai wa Uganda na Faith Cherotich wa Kenya.