Heko! Omanyala afuzu kwa nusu fainali licha ya kufika Marekani saa chache kabla ya mbio kuanza

Omanyala aliwasili Oregon takriban masaa matatu kabla ya mbio kuanza

Muhtasari

•Omanyala alipata Visa yake Alhamisi kisha kuanza safari na kuwasili Marekani takriban masaa matatu tu kabla ya mashindano.

•Licha ya kuwa na muda mfupi wa kujiandaa, Omanyala aliibuka wa tatu katika kundi hilo na kufuzu kwa nusu fainali.

akionyesha medali yake ya dhahabu kwenye picha ya maktaba
Bingwa wa Afrika katika mbio za mita 100 Afrika Ferdinand Omanyala akionyesha medali yake ya dhahabu kwenye picha ya maktaba
Image: PSCU

Bingwa wa Afrika katika mbio za mita 100, Ferdinand Omanyala alienda kinyume na kufuzu kwa nusu-fainali kwenye mashindano ya World Atletics Championship yanayoendelea katika jimbo la Oregon, Marekani licha ya kuwasili masaa machache tu kabla.

Safari ya mwanariadha huyo mwenye umri wa miaka 26 ya kuelekea Marekani ilitatizika kufuatia kucheleweshwa kwa Visa yake ya usafiri.

Alipata Visa yake Alhamisi kisha kuanza safari na kuwasili Marekani takriban masaa matatu tu kabla ya mashindano ya kufuzu semi fainali za mbio za mita 100 kung'oa nanga.

Omanyala aliwekwa katika kundi la saba ambalo lilikimbia Jumamosi mwendo wa saa kumi na moja asubuhi.

Licha ya kuwa na muda mfupi wa kujiandaa, Omanyala aliibuka wa tatu katika kundi hilo na kufuzu kwa nusu fainali.

Bingwa huyo alikamilisha mbio kwa sekunde 10.10 huku Abdul Hakim wa Japan akiongoza kundi la 7 kwa sekunde 9.98 na Edward Osei-Nketia wa New Zealand akichukua nafasi ya pili kwa sekunde 10.08.

Hatua ya semi fainali itafanyika Jumapili huku kukiwa na matarajio makubwa hasa miongoni mwa Wakenya kwa Omanyala kufuzu fainali.

Wakenya wameendelea kumpongeza mwanariadha huyo kwa fahari aliyoiletea taifa licha ya masaibu yaliyokumba safari yake.

Mapema wiki hii Omanyala alikuwa mwenye wasiwasi kwani hakujua hatima yake baada ya Visa yake kuchelewa.

Kufikia Jumanne bado hakuwa ameokea stakabadhi hiyo muhimu ya usafiri. Alieleza wasiwasi wake kupitia Instagram.

"Inasikitisha kuwa sijasafiri hadi Oregon bado na mbio za mita 100 ni baada ya siku mbili. Ucheleweshaji wa visa," Omanyala alisema Jumatano.

Bila kukata tamaa mwanariadha huyo aliendelea kufanya mazoezi katika uwanja wa Kasarani huku akisubiri Visa.

Hatimaye alipokea stakabadhi hiyo muhimu Alhamisi na safari yake ikaratibiwa jioni hiyo.