Kwa nini niliamua kukimbilia Bahrain sio Kenya -Winfred Yavi, Mshindi wa mbio za mita 3000 kuruka viunzi afunguka

Yavi alibainisha kuwa uamuzi wa kubadili utaifa uliibua hisia mbaya sana na maoni hasi, haswa kutoka kwa marafiki.

Muhtasari

•Yavi anasema alikuwa tayari kuwakilisha nchi yake ya kuzaliwa lakini kwa bahati mbaya hakuwahi kuchaguliwa kamwe.

•Yavi alisema kuwa licha ya kuwa na utaifa wa Bahrain, mara nyingi yuko Kenya kwani kuna hali ya hewa nzuri kwa mafunzo.

alishinda dhahabu katika mbio za mita 3000 kuruka viunzi na maji
Winfred Yavi alishinda dhahabu katika mbio za mita 3000 kuruka viunzi na maji
Image: HISANI

Mwanariadha mzaliwa wa Kenya anayewakilisha Bahrain, Winfred Yavi Mutile anasema alikuwa tayari kuwakilisha nchi yake ya kuzaliwa lakini kwa bahati mbaya hakuwahi kuchaguliwa kamwe.

Baada ya kushinda mbio za mita 3000 kuruka viunzi na maji katika mashindano ya  Zurich Diamond League mnamo Septemba 2023, mwanariadha huyo mzaliwa wa kaunti ya Machakos alifanya mahojiano na mwanahabari za mitandaoni ambapo alizungumza kuhusu ushindi wake na safari yake ya kukimbia.

Yavi alisema kabla ya kufanya uamuzi wa kuhamia Bahrain takriban miaka nane iliyopita, alifanya majaribio mengi ili kupata nafasi katika timu ya taifa ya Kenya lakini hakufanikiwa kwani kulikuwa na ushindani mkali.

"Nilikuwa nikienda kwa majaribio ya timu ya Kenya, na sikufuzu. Kuenda Bahrain kilikuwa kipaumbele cha kwanza, lakini nilikuwa tayari kuwakilisha nchi yangu,” Yavi alisema.

Aliongeza, "Ushindani ulikuwa mkali. Unajua hapa Kenya tuko na wanariadha wengi na pia kupata ile nafasi angalau uingie kwa timu ya Kenya, ndio unaweza kuingia kwa timu ya Kenya lakini unapata wanachagua watu wawili tu, kama wewe ni nambari mbili ama nne unakosa. Mimi nilikuwa tayari kabisa lakini nilikuwa nakosa nafasi.”

Mwanariadha huyo mwenye umri wa miaka 24 alifichua kuwa mwaka 2016, aliibuka nambari tatu katika majaribio ya mashindano ya kimataifa ya vijana lakini ni wanariadha wawili wa kwanza pekee waliochaguliwa kwenda kuiwakilisha nchi.

“Nilikuwa nimefanya kazi nyingi, nilikuwa nimetia bidii, hivyo ndivyo nilikuja nikapata nafasi hiyo (ya Bahrain) na nikaenda. Ilikuja kama kipaumbele cha kwanza,” alisema.

Yavi pia alifichua kwamba ili kupata nafasi ya kuenda Bahrain, aliunganishwa na Mkenya mmoja aliye katika tasnia ya michezo.

“Pia wazazi walikubali, na kocha pia alikubali na akanipeleka hapo,” alisema.

Mwanariadha huyo mwenye umri wa miaka 24 alithibitisha kuwa mbali na kuiwakilisha Bahrain katika riadha, pia ana utaifa wa nchi hiyo ya Asia.

Hata hivyo, alibainisha kuwa uamuzi wa kubadili utaifa uliibua hisia mbaya sana na maoni hasi, haswa kutoka kwa marafiki.

"Ilileta hasi nyingi. Nilikuwa nikiulizwa nina uhakika gani kama nitaenda na kukimbia vizuri. Ilikuwa ngumu. Kila mtu alikuwa anakuja na mambo tofauti ya kuniambia. Wengine walisema nisiende huko nitaumia . Wazazi walikuja tukaongea, tukakaa chini na kocha na watu wengine. Tulikuja na mmoja na tukakubaliana,” she said.

Yavi alisema kuwa licha ya kuwa na utaifa wa Bahrain, mara nyingi yuko Kenya kwani kuna hali ya hewa nzuri kwa mafunzo.