Bondia wa Afrika Kusini afariki katika pambano la ndondi

Muhtasari

•Mchezaji huyo alipambana na mwenzake Siphesihle Mntungwa kuwania taji la WBF All Africa uzani mwepesi siku ya Jumapili.

•Shirikisho la mchezo wa ndondi Afrika Kusini (BSA) lilithibitisha kuwa Buthelezi alifariki Jumanne jioni.

Image: BBC

Bondia wa Afrika Kusini Simiso Buthelezi amefariki dunia baada ya kuvuja damu kwenye ubongo kufuatia pambano la ndondi lililofanyika mwishoni mwa juma mjini Durban.

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 24 alipambana na mwenzake Siphesihle Mntungwa kuwania taji la WBF All Africa uzani mwepesi siku ya Jumapili, lakini pambano hilo la raundi 10 lilisitishwa na mwamuzi baada ya Buthelezi kuonekana kuwa kivuli cha mpinzani asiyeonekana.

Picha za pambano hilo zilimuonyesha Mntungwa akianguka kupitia kamba na kisha, baada ya pambano hilo kuanza tena, Buthelezi alisonga mbele kuelekea kwenye kona tupu ambapo alianza kupiga ngumi.

Mntungwa alitangazwa mshindi na baadaye Buthelezi alianguka na kukimbizwa hospitalini. Aliwekwa katika hali ya kukosa fahamu baada ya kugundulika alikuwa anavuja damu kwenye ubongo.

Shirikisho la mchezo wa ndondi Afrika Kusini (BSA) lilithibitisha kuwa Buthelezi alifariki Jumanne jioni katika taarifa iliyotolewa kwa pamoja na familia ya bondia huyo.

Buthelezi alitambuliwa kama "bondia mkubwa ambaye alikuwa mfano mzuri nje na ndani ya ulingo".

BSA pia ilisema itafanya ukaguzi huru wa matibabu wa tukio hilo.

"Katika hospitali Bw Buthelezi alipewa huduma bora zaidi lakini hata hivyo alifariki dunia," taarifa hiyo ilisema.