Ngumi ya 'Sugunyo' yampa gari Bondia Karim Mandonga

Ushindi dhidi Wanyonyi ni mechi ya kwanza kwa bondia huyo kucheza nje ya Tanzania,

Muhtasari

• Mandonga sasa anamiliki gari kwa mara ya kwanza alilozawadiwa leo na mmoja wa wadau wa ngumi Tanzania.

•Ushindi dhidi ya Mkenya Wanyonyi ni mechi ya kwanza kwa bondia huyo kucheza nje ya Tanzania.

Karim Mandonga
Image: BBC

Bondia Karim Mandonga wa Tanzania sasa anamiliki gari kwa mara ya kwanza alilozawadiwa leo na mmoja wa wadau wa ngumi Tanzania.

Vyombo vya habari vya ndani vimeripoti kuzawadiwa huko kwa Mandonga.

Bondia huyo mwenye maneno na tambo za mbwembwe amerejea nchini Tanzania baada ya kutoka Kenya alikokwenda kupigana kwa mara ya kwanza kwenye pambano lake lisilo la ubingwa dhidi ya Daniel Wanyonyi. Alishinda kwa TKO kwa ushindi uliompa heshima.

'Namshukuru Mungu nilicheza kama niko Tanzania, nilitangaza ngumi yangu ya kigeni ikitoka Ukraine inaitwa Sugunyo, nashukuru mwenyezi mungu kwa hatua aliyonipa', alisema Mandonga baada ya kukabidhiwa gari hiyo.

Ushindi dhidi ya Mkenya Wanyonyi ni mechi ya kwanza kwa bondia huyo kucheza nje ya Tanzania, alikofanikiwa kujaza ukumbi mkubwa wa KICC Nairobi. Inakadiriwa zaidi ya watu 2,500 walijitokeza kushuhudia pambano hilo la Mandonga na Wanyonyi.

'Ni mechi yangu ya kwanza kucheza, ya kuonyesha maajabu ya kuimbiwa nyimbo ya taifa, machozi yalinitoka, ni tukio kubwa', alisema.