Fahamu kazi kubwa ambazo Sonko amemuahidi Conjestina baada ya kutoka rehab

Sonko amesema Conjestina hatarejea nyumbani kwake Siaya baada ya kukamilisha matibabu.

Muhtasari

•Sonko ameahidi kumpa kazi Conjestina Achieng' punde baada ya kukamilisha kipindi chake cha matibabu katika kituo cha kurekebisha hali jijini Mombasa.

•Sonko alifichua kwamba wanapanga kumfungulia bondia huyo kituo cha mafunzo ya ndondi ambapo atakuwa akitoa mafunzo ya mchezo huo.

katika hospitali ya Mombasa Women Empowerment Network Hospital huko Miritini siku ya Jumamosi, Septemba 3, 2022.
Bingwa wa ndondi Conjestina Achieng na gavana wa zamani wa Nairobi Mike Sonko katika hospitali ya Mombasa Women Empowerment Network Hospital huko Miritini siku ya Jumamosi, Septemba 3, 2022.
Image: ONYANGO OCHIENG'

Aliyekuwa gavana wa kaunti ya Nairobi, Mike Sonko ameahidi kumpa kazi bondia wa zamani Conjestina Achieng' punde baada ya kukamilisha kipindi chake cha matibabu katika kituo cha kurekebisha hali jijini Mombasa.

Katika taarifa yake ya Jumatano, Sonko ambaye alifadhili matibabu ya Conjestina aliweka wazi kwamba lejendari huyo wa ndondi hatarejea nyumbani kwake Siaya baada ya kuruhusiwa kuondoka katika kituo hicho.

Mfanyibiashara huyo alibainisha kuwa amepanga jinsi Conjestina atakavyokuwa akipata riziki baada ya kuruhusiwa kuaga kituo cha Mombasa Women Empowerment Network  ambako amekuwa kwa takribani miezi minane.

"Atakuwa Msimamizi Msaidizi wa Usalama na Mkuu wa mabouncer wote wa kike katika Club Volume Mombasa mida ya usiku na saa za kilele/likizo," Sonko alisema Jumatano kwenye kurasa zake za mitandao ya kijamii.

Aliongeza, "Pia atahudumu kama mkufunzi mkuu katika kumbi zote za mazoezi katika vituo vyetu (Salama Bling Beach Resort, Kimeremeta Safari Lodge n.k...).

Gavana huyo wa zamani pia alifichua kwamba wanapanga kumfungulia bondia huyo kituo cha mafunzo ya ndondi ambapo atakuwa akitoa mafunzo ya mchezo huo ambao ulimtengenezea jina kubwa barani Afrika.

Siku ya Jumatano, mchanganuzi maarufu wa spoti, Carol Radull alitoa taarifa kuhusu maendeleo ya bondia huyo wa zamani ambapo alifichua kuwa kwa sasa hali ya mama huyo wa kijana mmoja imeimarika.

"Miezi nane katika kituo cha Mombasa na msichana wangu Conjestina Achieng anakaa vizuri!" alisema kwenye Instagram.

Mchanganuzi huyo wa spoti aliendelea kufichua kwamba baada ya kukamilisha kipindi chake cha matibabu katika kituo hicho, Bi Conjestina atakuwa na kibarua cha kuwafunza wacheza ndondi chipukizi.

"Kazi kwenye gym inamngoja baada ya kukamilisha ambapo atakuwa akiwafunza mabondia wadogo," Radull alisema.

Kufuatia hayo, alitoa shukrani za dhati kwa Mike Sonko kwa niaba ya bondia huyo wa zamani wa timu ya taifa ya Kenya.