logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Samuel Eto'o azidiwa na hisia baada ya kukutana na mchezaji mwenzake wa zamani aliyegeuka kuwa mlinzi

Eto’o aliguswa sana na tukio hilo na akamwelekeza msaidizi wake apange mkutano na rafikiye huyo ili waungane tena.

image
na Samuel Mainajournalist

Football25 January 2025 - 09:43

Muhtasari


  • Eto'o alikuwa mjini Douala kwa mhadhara wa Kundi la Ecobank alipokutana na rafiki yake wa zamani, mwanamume ambaye aliwahi kucheza naye kandanda.
  • Eto'o alitazama nyuma kwa muda mfupi kabla ya kuendelea, lakini kisha akasimama, akageuka tena, na kugundua kuwa ni rafiki wa zamani.


Nyota wa zamani wa Barcelona na timu ya taifa ya Cameroon, Samuel Eto’o hivi majuzi alikutana na mchezaji mwenzake wa zamani ambaye sasa anafanya kazi kama mlinzi katika mji wa Douala.

 Eto’o ambaye sasa ni Rais wa Shirikisho la Soka la Cameroon (FECAFOOT) alikuwa mjini humo kwa mhadhara wa Kundi la Ecobank alipokutana na rafiki yake wa zamani, mwanamume ambaye aliwahi kucheza naye kandanda.

 Katika video ya kihisia iliyosambazwa kwenye mitandao ya kijamii, Eto’o alionekana akiwa amezungukwa na mashabiki na wengine waliohudhuria na alikuwa akitoka nje ya ukumbi huo wakati mtu ambaye hakuwa amenaswa kwenye kamera alipoita jina lake.

 Mwanzoni, gwiji huyo wa soka wa Cameroon alitazama nyuma kwa muda mfupi kabla ya kuendelea, lakini kisha akasimama, akageuka tena, na kugundua kuwa ni rafiki wa zamani.

 Mwanamume huyo ambaye alivalia sare za mlinzi aliingia kwenye fremu ya camera na uso wa Eto’o ukang’aa baada ya kumtambua.

 Nyota huyo wa zamani wa Barcelona alionekana akimsalimia rafikiye kwa uchangamfu na mchezaji huyo mwenzake wa zamani, akamkumbatia kwa muda mfupi, na wakazungumza kwa raha kwa lugha ya Bassa’a, lahaja ya Kikameruni.

 Eto’o alionekana kuguswa sana na mara kwa mara akaupapasa mkono wa rafiki yake walipokuwa wakikumbushana.

 Wawili hao walikuwa na mazungumzo ya maana, wakikumbuka uzoefu wao wa awali katika uwanja.

 Akigeukia umati uliokusanyika karibu nao, Eto’o alimtambulisha mtu huyo, akisema, “Alikuwa mchezaji mwenzangu. Nilicheza naye.”

 Kipindi hicho cha kugusa hisia kimevutia watu wengi kwenye mitandao ya kijamii, huku watumiaji wengi wakimsifu Eto’o kwa unyenyekevu wake.

 Eto’o aliguswa sana na tukio hilo na akamwelekeza msaidizi wake kuweka miadi rasmi na rafiki yake wa zamani ili waungane tena.

 Eto’o, mmoja wa wanasoka wakubwa barani Afrika, alikuwa na taaluma kubwa, akishinda mataji manne ya Mchezaji Bora wa Mwaka wa Afrika na kuchezea vilabu maarufu vya Uropa kama vile Barcelona, ​​​​Inter Milan na Chelsea.

 Alipata mataji matatu ya kihistoria akiwa na Inter Milan mwaka 2010 na kushinda Ligi ya Mabingwa akiwa na Barcelona.

 Tangu alipostaafu mwaka wa 2019, Eto’o ameendelea kuwa na ushawishi mkubwa katika ulimwengu wa soka, na Desemba 2021, alichaguliwa kuwa Rais wa FECAFOOT, akiendelea kujitolea kuendeleza mchezo huo nchini Cameroon.


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved