EURO 2020:Italia, Ubelgiji, Uingereza, Uholanzi, Austria zang'aa

Mchuano kati ya Udenmarki na Ufini ambao ulichezwa saa moja usiku ulisitishwa kwa muda baada ya kiungo wa klabu ya Inter Milan na Udenmarki, Christian Eriksen, kupatwa na mshtuko wa moyo katika dakika ya 42 kwenye tukio la kuhofisha sana.

Muhtasari

•Tangu kuanza kwa michuano ya EURO 2020 siku ya Ijumaa, mechi saba zimechezwa tayari huku nchi bingwa katika bara Ulaya zikinyakua ushindi kwenye mechi zao za kwanza.

ENGLAND SQUAD
ENGLAND SQUAD
Image: HISANI

Michuano ya EURO 2020 ambayo  ilikuwa imesubiriwa kwa takriban miaka tano hatimaye ilianza Ijumaa iliyopita.

Kwa kawaida, kombe la EURO huwaniwa baada ya maika minne ila kwa mara hii michuano hiyo inachezwa baada ya miaka tano kwani mwaka jana iliahirishwa kutokana ujio wa virusi vya Korona.

Mara ya mwisho EURO kuchezwa ilikuwa mwaka wa 2016 huku nchi ya Ureno ikitwaa ushindi .

Tangu kuanza kwa michuano ya EURO 2020 siku ya Ijumaa, mechi saba zimechezwa tayari huku nchi bingwa katika bara Ulaya zikinyakua ushindi kwenye mechi zao za kwanza.

Mechi ya kwanza ilikuwa kati ya Uturuki na Italia ambapo mabingwa wa mwaka wa 1968, Italia, waliweza kuwaadhibu Uturuki mabao 3 kwa 0. Mabao ya Ciro Immobile, Lorenzo Insigne na Meril Demiral(Kujifunga) yalifanikisha ushindi huo.

Mechi tatu ziliweza kuchezwa siku ya  Jumamosi ya kwanza ikiwa kati ya Welisi na Uswisi ambazo zilipiga sare ya 1-1.  Keiffer Moore na Breel Embolo walifungia Welii na Uswisi mtawalia.

Mchuano kati ya Udenmarki na Ufini ambao ulichezwa saa moja usiku ulisitishwa kwa muda baada ya kiungo wa klabu ya Inter Milan na Udenmarki, Christian Eriksen, kupatwa na mshtuko wa moyo katika dakika ya 42 kwenye tukio la kuhofisha sana.

Hata hivyo, mechi hiyo iliweza kuendelea mwendo wa saa tatu unusu baada ya uthibitisho kuwa mchezaji huyo matata alikuwa amepata fahamu na hakuwa kwenye hatari tena. Hata hivyo, bao la Joel Ponjanpalo katika dakika ya 60 liliweza kusaidia Ufini kushinda mechi hiyo.

Wachezaji wa Udenmarki wazingira Eriksen baada ya kupatwa na mshutuko wa moyo
Wachezaji wa Udenmarki wazingira Eriksen baada ya kupatwa na mshutuko wa moyo
Image: Hisani

Mwendo wa saa nne usiku, Ubelgiji ilikaribisha Urusi kwenye mchezo wa kusisimua mno na kuweza kushinda 3-0 kupitia mabao mawili ya Romelu Lukaku na moja la Thomas Meunier.

Siku ya tatu, Jumapili, ilihusisha mataifa sita. Uingereza ilichapa Croatia bao 1-0  kupitia bao la mshambulizi wa Machester City Raheem Sterling katika dakika ya 57.

Mechi ya pili ilikuwa kati ya Austria na Makedonia ya Kaskazini ambapo mabao ya Stefan Lainer, Michael Gregoritsch na Marko Arnautovic yaliwezesha Austria kupata ushindi mkubwa wa 3-1. Bao la Makedonia lilifungwa na Goran Pandev.

Mechi  ya kusisimua kati ya Uholanzi na Ukrania ilifunga wikendi ambapo jumla ya mabao tano yalifungwa.

Georginio Wijnaldum,Wout Weghorst na Denzel Dumfries walifungia walipatia Uholanzi ushindi wa 3-2 huku mabao mawili ya Ukrania yakifungwa na Andriy Yarmolenko na Roman Yaremchuk.

Mechi zingine tatu zitachezwa usiku wa Jumatatu huku Uskoti ikikaribisha Ucheki, Upoli ikaribishe Slovakia huku mechi kubwa ikiwa kati ya Uhispania na Uswidi mwendo wa saa nne usiku.