EURO 2020: Ronaldo avunja rekodi; Ureno, Ufaransa zang'aa

Kufikia sasa, Ronaldo ameifungia nchi yake mabao 106 na huenda akavunja rekodi nyingine ya mchezaji aliyefungia nchi yake mabao mengi zaidi iwapo atafunga mabao manne tu zaidi michuano hiyo inapoendelea

Muhtasari

•Mabao mawili ya Ronaldo yalimsaidia kuvunja rekodi ya kombe hilo kwa kuwa mchezaji aliyefunga mabao mengi zaidi, 11, kwenye historia ya Kombe la EURO.

•Bao la Matt Hummels la kujifunga kwenye dakika ya 20  lilisaidia Ufaransa kuibuka mshindi

Christiano Ronaldo akisherehekea bao lake
Christiano Ronaldo akisherehekea bao lake
Image: Hisani

Siku ya tano ya Kombe la EURO 2020 ilihusisha mataifa manne kwenye kundi F.

Hungaria ilikaribisha Ureno ilhali Ujerumani ilikuwa mgeni wa Ufaransa. Michuano hiyo ambayo ilichezwa usiku wa Jumanne ilikuwa ya kusisimua mno.

Kwenye mechi ya kwanza ambayo ilichezwa mida ya saa moja usiku, Ureno ambayo ndiyo timu inayoshikilia kombe hilo ilikuwa inatazamia kuanza kulinda taji ambalo iliweza kunyakua mwaka wa 2016.

Mechi kati ya Hungaria na Ureno ilibaki sare tasa hadi dakika ya 84 wakati ambao mlinzi wa Borrusia Dortmund, Raphael Guerreiro alifungia nchi yake Ureno bao la kwanza.

Mabao mawili ya Christiano Ronaldo kwenye dakika ya 87 na 92 yalimsukuma hadi kileleni mwa jedwali la wafungaji bora  kuungana na Romelu Lukaku wa Ubelgiji na Patrik Schick wa Ucheki ambao wana mabao mawili kila mmoja pia.

Matt Hummels ajifunga
Matt Hummels ajifunga
Image: Hisani

Mabao hayo yalimsaidia kuvunja rekodi ya kombe hilo kwa kuwa mchezaji aliyefunga mabao mengi zaidi, 11, kwenye historia ya Kombe la EURO.

Rekodi hiyo ilikuwa imeshikiliwa na aliyekuwa mchezaji wa timu ya Ufaransa, Michel Platini ambaye alifunga Jjumla ya mabao 9 kwenye kombe la EURO.22

Kufikia sasa, Ronaldo ameifungia nchi yake mabao 106 na huenda akavunja rekodi nyingine ya mchezaji aliyefungia nchi yake mabao mengi zaidi iwapo atafunga mabao manne tu zaidi michuano hiyo inapoendelea. Ali Daei wa Irani ndiye anayeshikilia rekodi hiyo na mabao 109 kwa timu ya taifa lake.

Mechi ya pili ilikuwa baina ya mabingwa wa kombe la dunia mwaka wa 2014 na 2018, Ujerumani na Ufaransa mtawalia.

Bao la Matt Hummels la kujifunga kwenye dakika ya 20  lilisaidia Ufaransa kuibuka mshindi kwenye hiyo iliyojaa msisimko.  Hata hivyo, Mabao ya Kylian Mbappe na Karim Benzema yalikataliwa kwa madai kuwa walikuwa wameotea na kwa hivyo kupelekea mechi kuisha kwa 1-0, wenyeji Ufaransa wakiibuka washindi.

Timu za Ufini, Urusi, Uturuki, Welisi, Italia na Uswisi zitakuwa zinacheza mechi ya pili kila mmoja usiku wa Jumatano.