Mane atumia zaidi ya Sh67,300,000 kujenga hospitali katika kijiji chake cha Bambali, Senegal

Mwaka wa 2019 Mane alijenga shule ya upili kijijini hicho

Muhtasari

•Baada ya kujenga shule ya upili katika kijiji chake cha Bambali mwaka wa 2019, mchezaji huyo ambaye ana umri wa miaka 29 amejenga hospitali kubwa iliyomgharimu zaidi ya Sh67,300,000 katika kijiji hicho.

•Kando na shule na hospitali, Mane amejenga duka kubwa katika kijiji hicho huku ripoti zikisema kuwa ana nia ya kujenga uwanja mkubwa pale

Sadio mane na rais Macky Sall
Sadio mane na rais Macky Sall
Image: Hisani

Mshambulizi wa klabu ya Liverpool na timu ya taifa ya Senegal Sadio Mane ameendelea kuonyesha ushujaa na utu kwa raia wa  taifa lake.

Baada ya kujenga shule ya upili katika kijiji chake cha Bambali mwaka wa 2019, mchezaji huyo ambaye ana umri wa miaka 29 amejenga hospitali kubwa iliyomgharimu zaidi ya Sh67,300,000 katika kijiji hicho.

Mane alikutana na rais wa taifa hilo, Macky Sall kujadiliana kuhusu mradi huo mapema mwezi huu baada ya kushiriki kwenye mechi dhidi ya Zambia na Cape Verde. Aliomba serikali ya nchi hiyo kupeleka wahudumu wa afya katika hospitali hiyo.

Wiki chache baadae hospitali hiyo imezinduliwa rasmi na kupokezwa kwa serikali ya Senegal. Hospitali hiyo inadaiwa kuhudumia wakazi wa vijiji 34 ambazo ni jirani na  Bambali.

Kando na shule na hospitali, Mane amejenga duka kubwa katika kijiji hicho huku ripoti zikisema kuwa ana nia ya kujenga uwanja mkubwa pale.