United wamsajili tena mlinda lango Tom Heaton; Mata, Grant waongeza mkataba

United ilitangaza makubaliano ya kumsajili mshambulizi matata wa Borrusia Dortmund, Jadon Sancho siku ya Alhamisi

Muhtasari

•Mata amesifiwa sana na United kwa kuwapa motisha wachezaji wenye umri mdogo na anapendelewa sana na kocha Ole Gunnar Solskjaer.

•Heaton alipokuwa United wakati mwingi aliuzwa kwenye klabu mbalimbali kwa mkopo kati ya mwaka wa 2005 na 2010. 

Tom Heaton
Tom Heaton
Image: Twitter

Baada ya kutangaza makubaliano ya kumsajili mshambulizi matata wa Borrusia Dortmund, Jadon Sancho siku ya Alhamisi, klabu ya Manchester United imetangaza kumsajili tena mlinda lango Tom Heaton na kusainiwa kwa mkataba mpya na kiungo Juan Mata na mlinda lango Lee Grant.

Heaton, 35,  ambaye alikuwa katika klabu hiyo kwa kipindi cha miaka 13 kabla ya kusajiliwa rasmi na Cardiff City mwaka wa 2010 ametia saini mkataba wa miaka miwili hadi mwaka wa 2023.

United imempata mlinda lango huyo bure kwani mkataba wake na klabu ya Aston Villa ulikuwa umetamatika.

Heaton alipokuwa United wakati mwingi aliuzwa kwenye klabu mbalimbali kwa mkopo kati ya mwaka wa 2005 na 2010. 

Mwaka wa 2010 alinunuliwa na klabu ya Cardiff City. Baada ya hapo amechezea Bristol City, Burnley na Aston Villa hivi karibuni.

Kwa upande mwingine, kiungo wa kati Juan Mata amekubali kutia saini mkataba wa mwaka mmoja na klabu hiyo ya United.

Mata, 33, alisajiliwa kutoka Chelsea mwaka wa 2014 na amekuwa na kipindi kizuri sana na klabu hiyo yenye thamani na ufuasi  mkubwa sana. Kufikia sasa ameichezea United  mechi 273 na kufunga mabao 51.

Mata amesifiwa sana na United kwa kuwapa motisha wachezaji wenye umri mdogo na anapendelewa sana na kocha Ole Gunnar Solskjaer.

Mlinda lango, Lee Grant pia ametia saini mkataba mpya wa mwaka mmoja.

Grant, 38, alisajiliwa kutoka Stoke City mwaka wa 2018 ingawa hajachezeshwa sana na United kufikia sasa.