EURO 2020

Timu zipi zitafika fainali? EURO 2020 yaingia hatua ya semi fainali

Washindi wa mechi hizo wataingia fainali ya EURO 2020 ambayo itachezwa Jumapili ijayo.

Muhtasari

•Kombe hilo ambalo linahusisha mataifa ya  bara Ulaya iliingia katika hatua ya semi fainali baada ya mechi mbili za mwisho za hatua ya robo fainali kuchezwa usiku wa Jumamosi.

•Timu za Italia, Uhispania, Uingereza na Denmark zilihitimu kuingia hatua ya semi fainali. Mechi hizo zinatarajiwa kuchezwa mapema wiki ijayo.

Image: HISANI

Mashindano ya EURO 2020 yamebakisha hatua moja tu kufika fainali.

Kombe hilo ambalo linahusisha mataifa ya  bara Ulaya iliingia katika hatua ya semi fainali baada ya mechi mbili za mwisho za hatua ya robo fainali kuchezwa usiku wa Jumamosi.

Timu za Italia, Uhispania, Uingereza na Denmark zilihitimu kuingia hatua ya semi fainali. Mechi hizo zinatarajiwa kuchezwa mapema wiki ijayo.

Mabingwa mara tatu wa kombe la EURO, Uhispania walifuzu baada ya kuchapa Uswisi katika kipindi cha mikwaju ya penalti. Mechi hiyo iliisha sare ya 1-1 kwenye dakika 90 za  kawaida ilhali hakuna bao lolote lililoshuhudiwa kwenye dakika 30 za maongezi. Uhispania ilifunga penalti 3 wakati penalti 3 za Uswisi zilikataa kuingia ndani.

Mechi ya pili kuchezwa Ijumaa, mabingwa wa kombe hilo mwaka wa 1968, Italia walibandua Ubelgiji baada ya kuwapiga mabao 2 kwa 1 siku ya Ijumaa. Nicolo Barella na mshambulizi matata wa klabu ya Napoli Lorenzo Insigne walifungia Italia huku Romelu Luka wa klabu ya Intermilan akifungia Ubelgiji mkwaju wa penalti.

Mechi ya kwanza usiku wa Jumamosi ilikuwa kati ya Denmark na Ucheki. Denmark ambao wameendelea kuvuma katika michuano ya kombe la EURO licha ya kiungo wao muhimu, Christian Eriksen kuzirai uwanjani kwenye mechi ua kwanza waliwaangamiza Ucheki kwa mabao 2 kwa 1 na kuwawezesha kufuzu.

Mechi kati ya Uingereza na Ukraine ilikuwa ya kusisimua huku Uingereza ikiimarisha ndoto yake ya kushinda kombe la EURO kwa mara ya kwanza. Mabao mawili ya mshambulizi wa Tottenham, Harry Kane na bao la mlinzi wa Manchester United Harry Maguire na lingine la Jordan Henderson wa Liverpool yalipatia Uingereza ushindi wa 4-0.

Kwenye hatua ya semi fainali, Italia itamenyana na Uhispania usiku wa Jumanne huku Uingereza ikipambana na Denmark Jumatano usiku.

Washindi wa mechi hizo wataingia fainali ya  EURO 2020 ambayo itachezwa Jumapili ijayo.

Je, nani atafika fainali?