NANI GWIJI?

Nani gwiji? Messi kupimana nguvu na Neymar katika fainali ya Copa America 2021

Brazil na Argentina zitamenyana katika hatua ya mwisho siku ya Jumapili, saa tisa asubuhi masaa ya Afrika Mashariki.

Muhtasari

•Mechi ya kusisimua baina ya Argentina na Colombia ilichezwa mida ya saa kumi asubuhi katika umwanja wa Estadio Nacional de Brasilia nchini Brazil.

•Brazil ilishinda Peru bao 1-0 baada ya mshambulizi gwiji wa PSG, Neymar kumsaidia Lucas Paqueta wa Lyon kuifungia timu yao bao moja la kipekee katika dakika ya 35.

Image: HISANI

Hatimaye michuano ya  Copa America 2021 imeingia hatua ya fainali baada ya mechi ya mwisho ya semi fainali kuchezwa usiku wa kuamkia Jumatano.

Mechi ya kusisimua baina ya Argentina na Colombia ilichezwa mida ya saa kumi asubuhi katika umwanja wa Estadio Nacional de Brasilia nchini Brazil.

Mshindi wa mchuano huo aliamuliwa kupitia mikwaju ya penalti baada ya mechi kuishia sare ya 1-1 kwenye kipindi cha dakika 90 za kawaida.

Mshambulizi matata wa klabu ya klabu ya Barcelona, Lionel Messi alisaidia Lautaro Martinez wa Inter Milan kuifungia Argentina katika dakika ya saba kabla ya Luiz Diaz kuisawazishia Colombia katika dakika ya 61.

Dakika 120 za mchuano huo hazikutosha kuamua mshindi na ikalazimu mikwaju ya penalti kupigwa. 

Colombia walilemewa katika hatua hiyo huku ikifunga penalti mbili tu kati ya tano walizopiga ilhali Argentina walikosa kufunga penalti moja tu kati ya nne walizopiga.

Messi, Leandro Paredes na Lautaro Martinez walifungia Argentina huku penalti mbili za Colombia zikifungwa na Juan Cuadrado na Miguel Borja.

Mechi ya kwanza ya semi fainali kati ya Brazil na Peru ilichezwa mida ya saa nane usiku wa kuamkia Jumanne. 

Brazil ilishinda Peru bao 1-0 baada ya mshambulizi gwiji wa PSG, Neymar kumsaidia Lucas Paqueta wa Lyon kuifungia timu yao bao moja la kipekee katika dakika ya 35.

Brazil na Argentina zitamenyana katika hatua ya mwisho siku ya Jumapili, saa tisa asubuhi masaa ya Afrika Mashariki.

Peru na Colombia watang'ang'ania nafasi ya tatu na nne saa tisa asubuhi siku ya Jumamosi.

Je, nani ataibuka mshindi?