EURO 2020

FA yalaani vikali ubaguzi wa rangi unaoelekezwa kwa baadhi ya wachezaji wa Uingereza

FA imewakosoa wanaobagua wachezaji hao mitandaoni na kuwaarifu kuwa hawafai kuwa wafuasi wa timu hiyo.

Muhtasari

•Mwungano wa Kandanda Uingereza(FA) umelaani vikali vitendo vya ubaguzi wa rangi vinavyoelekezwa kwa baadhi ya wachezaji baada ya kupoteza mchuano wa fainali dhidi ya Italia usiku wa Jumapili.

•FA iliahidi kuwaunga mkono wachezaji walioathirika na kutaka wanaotekeleza uovu huo kupata adhab kali.

Kikosi cha Uingereza kikitayarisha kupiga mikwaju ya Penalti
Kikosi cha Uingereza kikitayarisha kupiga mikwaju ya Penalti
Image: TWITTER

Mwungano wa Kandanda Uingereza(FA) umelaani vikali vitendo vya ubaguzi wa rangi vinavyoelekezwa kwa baadhi ya wachezaji baada ya kupoteza mchuano wa fainali dhidi ya Italia usiku wa Jumapili.

Uingereza iliendeleza ukame wa miaka 55 bila taji kubwa baada ya kulemewa na mabingwa mara mbili wa kombe la FA, Italia kwenye kitengo cha penalti.

Matokeo hayo hayakufurahisha wengi wa mashabiki huku wengine wakitumia fursa hiyo kuelekeza ghadhabu yao kwa wachezaji watatu walioshindwa kufunga mikwaju yao ya penalti kwa njia zisizofaa.

Kupitia ujumbe wa kuchapishwa ambao ulitolewa mapema siku ya Jumatatu, FA imewakosoa wanaobagua wachezaji hao mitandaoni na kuwaarifu kuwa hawafai kuwa wafuasi wa timu hiyo.

"FA inalaani vikali ubaguzi wa namna yoyote na imeghadhabishwa na ubaguzi wa rangi mitandaoni unaoelekezwa kwa baadhi ya wachezaji wetu. Yeyote ambaye anatekeleza kitendo hicho kibaya hakubalishwi kufuata timu ya taifa" FA ilisema.

FA iliahidi kuwaunga mkono wachezaji walioathirika na kutaka wanaotekeleza uovu huo kupata adhab kali.

"Tutafanya lolote tuwezalo kuunga mkono wachezaji walioathirika na tunapendekeza adhabu kali kwa wanaotekeleza ubaguzi huo" FA ilisema.

Italia ilishinda Uingereza kwenye kipindi cha penalti kwa kutia nyavuni penalti tatu  huku Uingereza ikifaulu kufunga mbili tu.

Leonardo Bonucci, Domenico Berardi na Federico Bernadeschi walifungia Italia huku mikwaju ya Andrea Belotti na Jorginho ikosa kupita mikono ya mlinda lango wa Uingereza  Jordan Pickford.

Kwa upande wa Uingereza, Harry Kane na Harry Maguire waliweza kumfunga Gianluigi Donnarumma wa Italia huku mikwaju ya Marcus Rashford, Jadon Sancho na Bukayo Saka yote ikikosa kugusa nyavu.