Arsenal yajiondoa kwenye michuano ya kombe la Florida kufuatia kugunduliwa kwa visa vya Corona

Inadaiwa kuwa waliopatikana na virusi hawaonyeshi dalili zozote na wanaendelea kujitenga wakiwa nyumbani

Muhtasari

•Gunners walikuwa wasafiri kuelekea Marekani siku ya Jumatano ili kushiriki kwenye michuano ya kombe la Florida ambayo itaanza mnamo Julai 25.

•Kombe la Florida limeshirikisha klabu zingine kama Inter Milan ya Italia, Everton ya Uingereza na Millionarios ya Colombia.

Image: HISANI

Klabu ya Arsenal imesitisha ziara ya Marekani iliyokuwa imepangwa kufuatia visa kadhaa vya virusi vya Corona miongoni mwa kikundi kilichokuwa kinatarajiwa kuenda.

Gunners walikuwa wasafiri kuelekea Marekani siku ya Jumatano ili kushiriki kwenye michuano ya kombe la Florida ambayo itaanza mnamo Julai 25.

"Kufuatia idadi ndogo ya kesi za COVID miongoni mwa kikundi kilichokuwa kimepangwa kusafiri kesho kuenda Marekani, imebidi tujiondoe kwenye michuano ya kombe la Florida" Klabu hiyo ilitangaza kupitia tovuti yake rasmi.

Ingawa haikuwekwa wazi waliopatikana na virusi hivyo, inadaiwa kuwa hawaonyeshi dalili zozote na wanaendelea kujitenga manyumbani.

"Kwa sasa tunaendelea kufanya mipango mbadala ya kuendelea na matayarisho ya msimu mpya kulingana na mikakati ya ligi ya Premier." Gunners waliendelea kusema.

Kombe la Florida limeshirikisha klabu zingine kama Inter Milan ya Italia, Everton ya Uingereza na Millionarios ya Colombia.

Gunners walianza matayarisho ya msimu wa 2021/22  na ziara ya Uskoti ambapo walicheza mechi za kirafiki na klabu ya Rangers na ya Hibernian bila kupata ushindi wowote. 

Hibernian ilicharaza Gunners mabao mawili kwa moja huku mechi dhidi ya Rangers iliyochezwa Jumamosi ikiishia sare ya 2-2.

Ligi kuu Uingereza inapangwa kuanza mnamo tarehe 13 mwezi Agosti huku Arsenal ikimenyana na Brentford kwenye mechi yake ya kwanza.