FKF yatoza K'Ogalo na Ingwe faini ya milioni 10 kwa kutocheza mechi

Klabu hizo mbili ambazo zina ufuasi mkubwa sana nchini pia zilitolewa alama 3 kila mmoja kufuatia hayo

Muhtasari

•K'ogallo na Ingwe wametozwa faini ya milioni kumi kama malipo ya hasara ya gharama ya kupanga mechi iliyotumiwa na FKF

•Kamati ya utendaji ya FKF pia imeafikia kusimamisha kazi wenyekiti wa K'gallo na Ingwe, Ambrose Rachier na Dan Shikanda mtawalia wakisubiria adhabu zaidi.

Rais wa FKF Nick Mwendwa
Rais wa FKF Nick Mwendwa
Image: FKF

Shirikisho la soka nchini(FKF) ambalo linaongozwa na Nick Mwendwa limetoa adhabu kali kwa mashemeji Gor Mahia na AFC Leopards kwa kukosa kucheza mechi nambari  260 iliyokuwa imepangwa kuchezwa siku ya Jumamosi katika uwanja wa Thika.

K'ogallo na Ingwe wametozwa faini ya milioni kumi kama malipo ya hasara ya gharama ya kupanga mechi iliyotumiwa na FKF.

Ingwe ambao walikuwa wenyeji kwenye mechi hiyo watalazimika kulipa shilingi milioni 6 huku wageni wake Gor Mahia wakitozwa shilingi milioni 4.

Klabu hizo mbili ambazo zina ufuasi mkubwa sana nchini pia zilitolewa alama 3 kila mmoja kufuatia hayo.

Kulingana na FKF, sheria zinazoongoza mchezo wa soka nchini zasema kuwa iwapo timu zitakosa kuhudhuria na kucheza mechi iliyokuwa imepangwa basi alama tatu zitaondolewa kwa  aidha timu moja ama zote mbili na mabao mawili kutoka kwa yale ambayo yashafungwa. Adhabu zaidi pia yaweza tekelezwa.

"Hayo yakifanyika tena basi adhabu zaidi itatekelezwa dhidi ya klabu hizo mbili kwa kufuata sheria zinazoongoza mchezo wa soka nchini" FKF ilisema.

Mnamo Ijumaa wiki iliyopita klabu hizo mbili zilikuwa zimetishia kukosa kucheza mechi yao siku  ya Jumamosi zikilalamikia kutolipwa hiba ya milioni 3.

Kamati ya utendaji ya FKF pia imeafikia kusimamisha kazi wenyekiti wa K'gallo na Ingwe, Ambrose Rachier na Dan Shikanda mtawalia wakisubiria adhabu zaidi.