Aliyekuwa mshambuliaji wa Barcelona Lionel Messi amekubali kujiunga na PSG

Muhtasari
  • Lionel Messi amekubali kandarasi ya miaka miwili kujiunga na klabu ya PSG baada ya kuondoka Barcelona
Image: GETTY IMAGES

Lionel Messi amekubali kandarasi ya miaka miwili kujiunga na klabu ya PSG baada ya kuondoka Barcelona kwa ghafla kulingana na mwandishi wa Makala ya michezo BBC Guillem Balague

Makubaliano hayo , ambayo yana kipengee cha kumruhusu Messi kuhudumu kwa mwaka wa tatu yatategemea matokeo ya vipimo vya matibabu.

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 34 ambaye pia ni nahodha wa timu ya taifa ya Argentina aliondoka Barcelona, klabu ya pekee ambayo ameichezea baada ya kushindwa kumpatia kandarasi mpya kutokana na masharti ya Fair Play ya ligi ya La liga.

Mkufunzi wa PSG Mouricio Pochettino aliongoza PSG kumaliza katika nafasi ya pili nyuma ya klabu ya Lille katika ligue 1 msimu uliopita.

''Imethibitishwa . Lionel Messi atakuwa mchezaji wa PSG'' , Ballague aliambia BBC Radio 5 .

''Ni hivyo ishafanyika. Imefanyika dakika chache zilizopita''.

"Kwa sasa kuna maafisa wengi wa polisi sawa na mashabiki uwanjani. Kila kitu kinaelekea kubadilika hivi punde. Kuna kamera nane hapa , lakini hilo litabadilika. Inaonekana kana kwamba ni kandarasi ya miaka miwili na mwaka mmoja wa nyongeza''.

''Wazo lake lilikuwa kuandikisha kandarasi hiyo Barcelona lakini sasa itakuwa PSG. Lakini iwapo anahisi vyema ataongeza mwaka mmoja zaidi pengine. Lakini lengo lake kuu ni kuwa PSG na baadaye kufanya vyema katika kombe la dunia la Qatar''.

Akifahamika kama mmoja ya wachezaji bora wa wakati wote, Messi alifunga magoli 672 katika mechi 778 akiichezea Barcelona , klabu aliojiunga nayo akiwa na umri wa miaka 13.

Alishinda taji la Ballon d'Or mara sita na kubeba mataji 35 akiwa na klabu hiyo ya Catalan.

Usajili wa Messi - ambaye anafaa kukutana na mchezaji mwenza wa zamani Neymar katika klabu hiyo ya Parc des Princes - ni mojawapo ya sajili bora zaidi katika historia ya soka.

Atacheza katika safu ya mashambulizi yenye nyota watatu, Neymar na Kylian Mbappe - wachezaji wanaodaiwa kuwa ghali zaidi duniani.

Iwapo hakutakuwa na matatizo yoyote , atakuwa mchezaji wa nne kuhamia PSG bila malipo msimu huu baada ya kuwasili kwa kiungo wa kati wa Uholanzi Georginio Wijnaldum, beki wa Uhispania Sergio Ramos na kipa wa Itali Gianluigi Donnarumma.

Beki wa kulia wa Morocco Achraf Hakimi pia alijiunga na klabu hiyo kutoka Inter Milan.

PSG bado haijashinda kombe la klabu bingwa Ulaya katika kipindi cha muongo mmoja licha ya kufanya uwekezaji wa kiwango kikubwa, huku mechi ya fainali dhidi ya Bayern Munich mwaka 2020 katika kombe hilo ikiwa ndio fursa ya karibu zaidi walioafikia.

Balague anasema: Kile ambacho wamiliki wa PSG wanataka ni kuiona timu yao katika fainali ya klabu b ingwa kila mwaka.

''Ukiwa na Messi una fursa kubwa. Pochettino akiwa msimamizi wa klabu hiyo na kandarasi yake ikiongezwa ina maana kwamba wana wazo la kupata ufanisi huo na Messi atafanikisha hilo''.

''Watashinda ligi, hiyo watapata licha ya kwamba walipoteza taji hilo msimu uliopita. Haitakuwa ligi yenye ushindani mkubwa, ikimaanisha kwamba atakuwa freshi kupambana katika kampeni ya kombe la klabu bingwa''.