Bruno Fernandes, Paul Pogba wang'aa huku Mashetani Wekundu wakipata ushindi wa 5-1 dhidi ya Leeds

Manchester United iko kileleni mwa jedwali la EPL huku mechi zingine sita zikitarajiwa kuchezwa hivi leo.

Muhtasari

•Vijana wa Ole Gunnar Solskjær waliwakaribisha Leeds katika mechi yao ya kwanza msimu wa 2021/22 Jumamosi mida ya saa nane unusu masaa ya Afrika Mashariki.

•Mabao matatu ya kiungo mahiri Bruno Fernandes, moja la mshambulizi Mason Greenwood na lingine la Fred yalisaidia washindi hao mara tatu wa ligi kuu ya Uingereza kuandikisha ushindi wao wa kwanza msimu huu.

Image: TWITTER//MANCHESTER UNITED

Klabu ya Manchester  imeandikisha ushindi mkubwa wa 5-1 dhidi ya Leeds United ugani Old Trafford.

Vijana wa Ole Gunnar Solskjær waliwakaribisha Leeds katika mechi yao ya kwanza msimu wa 2021/22 Jumamosi mida ya saa nane unusu masaa ya Afrika Mashariki.

Mabao matatu ya kiungo mahiri Bruno Fernandes, moja la mshambulizi Mason Greenwood na lingine la Fred yalisaidia washindi hao mara tatu wa ligi kuu ya Uingereza kuandikisha ushindi wao wa kwanza msimu huu.

Mchezaji mwingine aliyeonyesha ubora wake katika mechi hiyo ni kiungo wa kati Paul Pogba ambaye alisaidia katika mabao manne yaliyofungwa na mashetani wekundu.

Mlinzi Luke Ayling alifungia Leeds bao lake la pekee akisaidia na mlinzi mwenzake Stuart Dallas.

Manchester United iko kileleni mwa jedwali la EPL huku mechi zingine sita zikitarajiwa kuchezwa hivi leo.

Burnley watakaribisha Brighton mida ya saa kumi na moja, Chelsea wachuane na Crystal Palace, Everton wamenyane na Southampton, Leicester wakaribishe Wolves, Watford wacheze dhidi ya Aston Villa huku mechi ya mwisho kati ya Norwich na Liverpool ikichezwa saa moja unusu.