EPL 2021/22: Matokeo ya kusisimua na ya kushangaza yaandikishwa katika mechi za ufunguzi wa ligi

Kwa sasa Manchester United, Chelsea, Liverpool na West Ham zinashikilia nafasi ya kwanza, pili, tatu na ya nne mtawalia huku Arsenal, Crystal Palace, Norwich na Leeds zikikalia nafasi nne za mwisho mtawalia

Muhtasari

•Mchuano kati ya Brentford na Arsenal  ambao ulichezwa usiku wa Ijumaa ulifungua rasmi msimu wa 2021/22 wa ligi kuu.

•Manchester United kwa sasa inaongoza jedwali la EPL baada ya kupata ushindi mkubwa wa 5-1 dhidi ya Leeds United. 

•Licha ya City kutumia pesa nyingi zaidi kuimarisha kikosi hawakuweza kuzuia vijana wa Nuno Espirito kupata ushindi wa 1-0. Bao la pekee la Son Heung-Min katika dakika ya 55 lilisaidia klabu hiyo ya London kuzima moto wa washindi wa ligi msimu uliopita

Tottenham washerehekea bao la Son
Tottenham washerehekea bao la Son
Image: HISANI

Wiki ya kwanza ya ligi kuu Uingereza (EPL) imeshuhudia mechi 10 za kusisimua  na zingine za kushangaza. 

Mchuano kati ya Brentford na Arsenal  ambao ulichezwa usiku wa Ijumaa ulifungua rasmi msimu wa 2021/22 wa ligi kuu.

Brentford ambao walipandishwa ngazi kutoka Championship msimu uliopita walishangaza wengi baada ya kuzima Wanabunduki kwa mabao 2-0.

Matokeo hayo yameibua ghadhabu kutoka kwa mashabiki wa Arsenal ikiwemo rais wa Rwanda Paul Kagame ambao wameshinikiza mabadiliko kufanyika klabuni.

Mechi saba  za kusisimua zilichezwa siku ya Jumamosi.

Manchester United kwa sasa inaongoza jedwali la EPL baada ya kupata ushindi mkubwa wa 5-1 dhidi ya Leeds United. Viungo wa kati wa Mashetani Wekundu  waling'aa kwenye mechi huku Bruno akifunga mabao matatu naye Pogba akisaidia katika maboa manne kati ya tano yaliyofungwa.

Chelsea ilinyuka Crystal Palace mabao matatu kwa sufuri , Everton ikacharaza Southampton 3-1, Leicester ikapata ushindi wa 1-0 dhidi ya Wolves, Burnley ikachapwa na Brighton 1-2 huku Watford ambao pia walipandishwa ngazi mwaka huu wakishangaza wengi kwa kupiga Aston Villa 3-2 licha ya Villa kutia juhudi kubwa katika kuboresha kikosi chake.

Mechi ya mwisho siku ya Jumamosi ilikuwa kati ya Liverpool na Norwich ambapo vijana wa Jurgen Kloop walipata ushindi wa mabao matatu bila majibu.

Mechi mbili zilichezwa siku ya Jumapili ambapo mchuano mkubwa kati ya Tottenham na mabingwa wa EPL msimu uliopita uliandikisha matokeo ya kushangaza.

Licha ya City kutumia pesa nyingi zaidi kuimarisha kikosi hawakuweza kuzuia vijana wa Nuno Espirito kupata ushindi wa 1-0. Bao la pekee la Son Heung-Min katika dakika ya 55 lilisaidia klabu hiyo ya London kuzima moto wa washindi wa ligi msimu uliopita.

Kwa sasa Manchester United, Chelsea, Liverpool na West Ham zinashikilia nafasi ya kwanza, pili, tatu na ya nne mtawalia huku Arsenal, Crystal Palace, Norwich na Leeds zikikalia nafasi nne za mwisho mtawalia.