"Mtasalia moyoni mwangu" Christiano Ronaldo aaga Juve kwa ujumbe maalum anapojiandaa kujiunga na United

Mashetani Wekundu watakamilisha uhamisho wa Ronaldo baada ya makubaliano ya masharti ya kibinafsi, vipimo vya kidakatari na kupokea kwa Visa.

Muhtasari

•Ronaldo amesema kuwa amefurahia kipindi cha miaka miwili ambacho amekuwa Juve na kudai kuwa klabu hiyo itasalia moyoni mwake milele.

Image: INSTAGRAM// CHRISTIANO

Ni dhahiri kuwa nyota wa soka duniani Christiano Ronaldo atajiunga na klabu ya Manchester United msimu huu.

Siku ya Ijumaa, United ilitangaza kurejea kwa mchezaji huyo matata ugani Old Trafford baada ya miaka 12.

Mashetani Wekundu watakamilisha uhamisho wa Ronaldo baada ya makubaliano ya masharti ya kibinafsi, vipimo vya kidakatari na kupokea kwa Visa.

Mamilioni ya mashabiki pamoja na wachezaji wa United ikiwemo Bruno Fernandes, Harry Maguire, Jesse Lingard na Raphael Varane wamemkaribisha nyumbani mshindi huyo wa tuzo la Ballon d' Or mara tano.

Kwa upande wake, Christiano ambaye aliondoka Juventus asubuhi ya Ijumaa ameaga mabingwa hao wa Italia kwa ujumbe maalum.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Ronaldo amesema kuwa amefurahia kipindi cha miaka miwili ambacho amekuwa Juve na kudai kuwa klabu hiyo itasalia moyoni mwake milele.

"Leo naondoka kutoka kwa klabu ya ajabu, kubwa zaidi Italia na mojawapo wa klabu kubwa zaidi bara Ulaya. Nimepatiana moyo wangu na roho kwa Juventus na nitaendelea kupenda jiji la Turin hadi siku zangu za mwisho.

'Tifosi Bianconeri' wamekuwa wakiniheshimu kila mara na nimejaribu kuwashukuru kwa heshima hiyo kwenye kila mechi, kila msimu na kila mashindano. 

Hatimaye, sote tunaweza kuangalia nyuma na kugundua kuwa tumeshinda vitu kubwa, sio tuliyoyataka ila tuliandika hadithi nzuri pamoja.

Nitaendelea kuwa mmoja wenu. Nyinyi sasa ni sehemu ya historia yangu, kama ninavyojihisi kuwa ssehemu ya historia yenu. Italia, Juve, Turin, Tifosi, Bianconeri, mtasalia moyoni mwangu" Ronaldo aliandika.

Mshambuliaji huyo anatazamiwa kujiunga rasmi na United hivi karibuni baada ya kukamilika kwa utaratibu wa usajili.